
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano, imesema itaunda tume ya kuchunguza askari wasio waaminifu wanaodaiwa kujihusisha na uchukuwaji rushwa na kusababisha kupitishwa kwa dawa za kulevya katika visiwani vya Zanzibar.
Naibu Waziri wa mambo ya ndani Tanzania, Yussuf Hamad Masauni, alisema hayo huko makao makuu ya Polisi Ziwani wakati alipozungumza na vyombo vya habari kufuatia ongezeko la uingizaji wa dawa za kulevya Zanzibar.
Alisema serikali haijaridhishwa na kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya inayochukuliwa na polisi kwa upande wa Zanzibar.
Alisema ongezeko la uingizaji wa dawa za kulevya linatokana na baadhi ya askari wasio waaminifu kupokea rushwa na kuridhia kuingizwa kwa dawa ya kulevya hali inayopelekea kuwapa mwanya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuendelea kuingiza biashara hiyo.
Alisema tume hiyo itakapokuja itachukua vielelezo vilivyopo ili kupata urahisi wa kuwatambua askari hao kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria.
“Tunataka tupate mtandao wote wa askari wanaochukua rushwa, hatuwezi kumvumilia askari anayeruhusu kuingizwa dawa za kulevya visiwani mwetu”, alisema Masauni.
Masauni alichukizwa na watendaji wasio waaminifu kwa kuendelea kuruhusu kuingizwa dawa za kulevya hali inayopelekea kuharibika kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya na kupelekea vijana kupoteza mwelekeo wao wa maisha.
“Hili jambo linaniumiza rohoni kuona vijana wetu wanapoteza mwelekeo wao kwa kutumia dawa za kulevya”, alisema Masauni.
Alisisitiza kuwa jeshi hilo halitowavumilia askari ambao hawafanyi wajibu wao ipasavyo na kuipeleka Zanzibar kuwa chaka la kuingiza dawa za kulevya.
“Hatuwezi kuendelea kukaa na Askari ambao hawafanyi wajibu wao tukastahamili tu, hadi leo kisiwa chetu kinashindwa kudhibiti dawa za kulevya tunatumia mwamvuli wa kujificha kupambana na dawa za kulevya kwa kutumia wahalifu”, alisema.
Zanzibarleo.
Comments