‘Msiwafungie watoto walemavu’.

WAZAZI na walezi wameaswa kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu na badala yake walelewe, kutunzwa na kuendelezwa kupitia nyanja mbali mbali.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa hospitali ya Tasakhta Global, Tamima Hassan Abdalla Turky, wakati akizungumza na wazazi na walimu wa watoto hao walipofika kwa ajili ya kupatiwa matibabu ikiwa ni kuadhimisha miaka minne tokea kuanzishwa hospitali hiyo.
Alisema, watu wenye ulemavu ni sehemu ya binaadamu na wanastahiki haki na heshima kama ilivyo kwa binadamu wengine.
Aidha, alisema watoto wenye ulemavu, wanakuwa na vipaji na uwezo wa kufanya mambo makubwa katika jamii.
Mbali na hayo, aliwasisitiza wazazi kuacha kuwaficha watoto wa aina hiyo na kuwadharau badala yake kuwatoa katika jamii ili waweze kupata haki zao.
Aliziomba taasisi nyengine kujitokeza kuwasaidia watoto hao kwani wana mahitaji mengi ikiwemo matibabu na misaada mengine muhimu.
Daktari Dhamana wa hospitali hiyo, Ismail Ashrak, alisema watoto hao wanatakiwa kulelewa katika mazingira mazuri na salama hasa katika kuwapa vyakula bora ambavyo havitaleta madhara kwa afya zao ikiwemo mboga.
Alisema ni jambo la msingi kwa wazazi na walezi kuacha kuwapa vyakula vya makopo, chipsi na vyengine ambavyo vinawasababisha miili yao kuwa mikubwa na kuathiri afya zao.
Zubeida Ahmed Abdalla, Mwalimu wa kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili skuli ya Mwembemakumbi, aliupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa uamuzi wa kutoa matibabu kwa watoto hao kwani wengi wao afya zao hazipo vizuri.
Watoto hao wamepatiwa matibabu mbalimbali ikiwemo moyo, macho, masikio na maradhi mengine.
Zanzibarleo.

Comments