
KIWANDA cha sukari Mahonda, kimesimamisha uzalishaji wa sukari kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha na uzalishaji huo utaendelea Julai mwaka huu.
Meneja biashara wa kiwanda hicho, Pranav Shah, alisema uzalishaji huo kwa hatua ya awali ulianza Januari 21 hadi Aprili, ambapo uzalishaji ulisimamishwa.
Alisema kwa kawaida kipindi cha mvua miwa huwa inanyonya maji mengi hivyo inakosa uwezo wa kuzalisha sukari.
Alisema katika kipindi cha Januari uzalishali ulipositishwa mwezi Aprili, tani 3,300 za sukari zilizalishwa ambapo matarajio yao kwa mwaka huu ni kuzalisha tani 8,000.
Alisema kwamba lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa hiyo unakua endelevu na kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, alisema bado ni mapema kufikia uzalishaji huo kutokana na miwa kutopatikana kwa wingi.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kulima miwa ili kukisaidia kiwanda hicho kutimiza lengo lake la kuzalisha tani 30,000 za sukari kwa mwaka.
“Mahitaji ya kiwanda ni kuwa na ekari 11,000, juhudi mbalimbali zinafanywa na serikali kuhakikisha wananchi wanalima miwa kwa wingi ili kupata mali ghafi ya kutosha,” alisema.
Zanzibar24.
Comments