Dr. Shein anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi Maadhimisho ‘May Day’ Paje.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani mwaka huu zinazotarajiwa kufanyika kiwanja cha Paje.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi Mohammed, aliyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari kuelekea siku ya wafanyakazi duniani.
Alisema sherehe za Mei Mosi mwaka huu zitafanyika Paje ikiwa ni utaratibu wa kuzizungusha kufanyika kila mkoa hali inayowapa nafasi wananchi kuzishuhudia sherehe hizo.
Alisema maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na shamra shamra na mambo mbali mbali ikiwemo, bonanza la michezo, usafi wa mazingira katika sehemu za Mkoa wa Kusini Unguja, kutembelea wastaafu.
Alisema mwaka uliopita kumekuwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo kuwepo kwa jitihada zilizochukuliwa na serikali katika kuhakikisha hali ya amani na utulivu ya Zanzibar inaendelea.
Alisema jitihada iliyochukua serikali ya kuimarisha miundombinu ya nchi na huduma za jamii, ikiwemo barabara, kuendelea kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa wazee, vijana na watu wenye ulemavu nchini kwa kutunga sheria na sera za kuwatatulia matatizo yao.
Alisema jitihada nyengine kuimarisha vitengo vya kushughulikia na kutatua migogoro ya kikazi, na matatizo ya wafanyakazi yanayojitokeza katika sekta ya umma na binafsi, pamoja na kuanzisha kampeni maalum ya kupinga vita udhalilishaji.
Alisema mafanikio mengine ni kuongezwa pencheni ya kima cha chini kwa wastaafu na kuendelea kutoa pencheni ya wazee wote wa Zanzibar, pamoja na mpango wa uimarishaji wa taarifa za wananchi na uwajibikaji mpya wa wananchi ambao taarifa zao hazikupatikana katika kuimarisha mipango ya maendeleo ya nchi.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kumejitokeza changamoto katika sekta ya ajira kwa mwaka 2018/19 ambapo moja ya hizo kuna  ushirikishwaji mdogo wa vyama vya wafanyakazi katika vikao vya maamuzi sehemu za kazi.
Alisema shirikisho hilo limeweza kuwasilishwa karibu kesi 500 ambapo kati ya hizo moja tu imepatiwa ufumbuzi katika kamati ya usuluhisho.
Alisema changamoto nyengine kufutwa kwa malipo ya saa za ziada (over time) na likizo za mwaka bila sababu za msingi, matumizi mabaya ya sheria kwa baadhi ya wakuu wa taasisi na kuwasimamisha kazi au kuwaachisha kazi wafanyakazi bila ya sababu za msingi.
Changamoto nyengine alisema, mazingira hatarishi kwa baadhi ya wafanyakazi wanaotumia mashine za mionzi bila kulindwa kiafya na kiusalama, ugatuzi na tahadhari zake ikiwemo uhaba wa wafanyakazi.
Hivyo aliwataka wananchi wote kuviunga mkono vyama vya wafanyakazi katika jitihada zake za kuwaangunisha wafanyakazi kudai na kutetea na kulinda haki zao.
Katibu huyo alisema sherehe za mwaka huu zimebeba ujumbe usemao, ‘kuimarika kwa uchumi wa taifa kuendane na kuongezeka kwa maslahi ya wafanyakazi’.

Comments