
Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia, alieleza hayo jana wakati akifungua mkutano wa kujadili mkakati na changamoto zilizopo katika sekta ya utalii uliofanyika katika hoteli ya Madinat al Bahar iliyopo Chukwani.
Alisema ni vyema kwa wadau hao, kutoa taarifa sahihi kwa wageni zinazohusiana na masuala ya utalii sambamba na kutumia vyema maeneo ya kihistoria yaliopo nchini, kwani itasaidia kutumia fursa ya masoko hayo.
Pia aliwataka wadau hao, kuhakikisha wanalipa kodi na kufuata sheria za nchi ili ukusanyaji wa mapato eneo hilo uwe endelevu sambamba na kuwa eneo muhimu linaloendelea kuchangia vizuri pato la taifa.
Alisema utalii ni sekta muhimu ambayo inachangia kwa asilimia 27 ya Pato la taifa na asilimia 70 za fedha za kigeni zinazotokana na sekta hiyo, hivyo ni wajibu wa kila mdau kusimamia vyema utoaji wa huduma kwa maslahi binafsi na taifa kwa jumla.
“Sitokuwa tayari kuona uchumi wa Zanzibar unashuka mikononi mwangu kutokana na baadhi ya watu kutolipa kodi na kutofuata sheria na miongozo ya nchi”, alisema.
Sambamba na hilo, alisema hatomvumilia mtu yoyote ambae atabainika kuharibu historia ya Zanzibar hasa ikizingatiwa ni mojawapo ya eneo muhimu lenye kuongeza kasi ya uingiaji wa wageni nchini.
Alisema moja ya changamoto inayojitokeza kwa watembeza watalii wasiokuwa rasmini ni ukosefu wa maandalizi mazuri kwa wageni wanaofika nchini sambamba na baadhi ya taasisi zilizopo kisheria kutozingatia sheria za nchi.
Kuhusu usalama alisema ni jambo muhimu na linapaswa kupewa kipaumbele kwa kila mdau badala ya kuona biashara ndio kielelezo tosha cha maslahi yake.
Katika hatua nyengine aliwahimiza mawaziri wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kusimamia na kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi hasa ikizingatiwa ndio dira sahihi ya kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
zanzibarleo
Comments