Balozi Amina: Serikali kuimarisha mazingira ya viwanda.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema itahakikisha inaweka mazingira mazuri kwa viwanda vilivyokuwepo nchini ili viweze kuzalisha na kuongeza soko la ajira kwa wakulima.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha ZOFSO kinachozalisha mafuta ya alizeti mafuta ya mchikichi na bidhaa nyengine cha Saateni na kiwanda cha ZANTO kinachozalisha ‘tomato sauce’ na ‘chilli sauce’ cha Shakani.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuweka na kuhamasisha wawekezaji wa sekta hiyo nchini kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija kwa wananchi.
Aidha, alisema lengo la kufanya ziara hizo ni kuona uhakika wa viwanda hivyo vinafanya kazi na kuhakikisha wanasikiliza changamoto zinazowakabili ili kuweza kufanyiwa kazi.
Alisema wameanza ziara hiyo kuangalia mambo ya kilimo kwani kilio kikubwa cha wakulima kukosa soko hasa kilimo cha tungule sambamba na bidhaa hizo kwa kiasi kikubwa zitaweza kuwa na soko kubwa nje ya nchi.
Balozi Amina alisema hivi sasa serikali imeweka nguvu zake kuhakikisha viwanda vinakuwa na soko la ndani na pia kuweza kuuza bidhaa zao nje ya Zanzibar.
Sambamba na hayo, alisema kiwanda cha Tomato kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuwashajihisha wakulima kulima zaidi na kuweza kukiuzia kiwanda hicho ili kiweze kuzalisha kwa uhakika.
Wakati huo huo, Waziri Amina, akizungumza katika kiwanda cha ZOFSO Gulioni alisema kuzalishwa kwa mafuta ya alizeti kutasaidia sana kupunguza kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya Zanzibar.
Aliahidi, serikali itahakikisha inatoa msaada kwa kiwanda hicho ili kiendelee kuwasaidia wananchi na mpangilio kwa wananchi kupata bidhaa nyengine ya kilimo kwa Unguja na Pemba.
Zanzibarleo.

Comments