
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amesema Wizara yake inatekeleza agizo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk Ali Mohamed Shein kwa kukuza uzalendo, kuamsha ari na kuwaelimisha wanafunzi wote kuitambua historia ya nchi yao.
Akizindua "mpango wa nchi yetu ni urithi wetu" huko Dole wilaya ya maghribi A amesema kufanya hivyo ni kuwajenga wanafunzi kuwa wakakamavu , wenye nidham na maadili mema yenye kuzingatia mila, silka, desturi na utamaduni kwa mustakabali wa maisha yao na Taifa kwa ujumla.
Amesema Zanzibar ni nchi salama kwa wageni na wenyeji kwa wakati wote hivyo amewataka vijana kuitunza amani iliyopo kwa faida yao na vizazi vijavyo na kuwa mfano bora duniani kote.
Mhe Riziki amewaagiza walimu wote kuhakikisha wimbo wa Taifa wa Zanzibar na wa Tanzania pamoja na wimbo wa mashujaa zinaimbwa kila siku wakati wa paredi kabla ya wanafunzi kuingia madarasani.
Pia amewataka kuhakikisha katika kila skuli ya Serikali na binafsi ni lazima kuwepo nembo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na bendera ya Zanzibar zilizochorwa vizuri na kuwekwa pahala ambapo kila mtu anaziona.
Hata hivyo amewataka Walimu wakuu kuwatumia walimu wa ushauri nasaha, walimu wa dini, kamati ya skuli, masheha na watu wengine kwa nafasi zao kuwapatia nasaha na maelekezo mema wanafunzi katika utaratibu utakaoandaliwa na skuli na kuwapatia Elimu kuhusu udhalilishaji ili waweze kujitambua na kuendeleza utamaduni wa kizanzibar.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dkt.Idrisa Muslim Hija amesema Zanzibar ni nchi yenye sifa njema ikiwemo watu wakarimu na vivutio mbalimbali vya utalii hivyo ni lazima vitunzwe ili na kizazi kijacho kipate urithi mwema.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya michezo na utamaduni Bwana Hassan Tawakali Khairallah amesema jitihada za awali zimefanyika za kuwasilisha na kuelekeza maafisa Elimu wa mkoa na wilaya kuhakikisha walimu wakuu na walimu wengine wanasomesha na kuwalea vijana katika misingi imara ya kuwa raia wema na wazalendo kwa nchi yao.
Katika uzinduzi wa mpango huo kauli mbiu kwa mwaka huu ni "Nchi yetu ndio urithi wetu".




Comments