Walioaga dunia kwa mafuriko Malawi wafika 28 huku maelfu wakiwa katika hali mbaya.

Walioaga dunia kwa mafuriko Malawi wafika 28 huku maelfu wakiwa katika hali mbaya
Idadi ya watu walioaga dunia baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko kusini mwa Malawi imefikia 28 huku idadi ya raia walioathiriwa na maafa hayo ya kimaumbile ikiripotiwa kuongezeka maradufu.

Chipiliro Khamula Msemaji wa Kitengo cha Kukabiliana na Maafa katika Wizara ya Usalama wa Ndani ya Malawi  amesema kuwa Juzi Jumamosi watu 28 walithibitishwa kuaga dunia kufuatia mafuriko hayo yaliyoikumba nchi hiyo na wengine 124 kujeruhiwa. 
Ijumaa iliyopita Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi alitangaza hali ya maafa katika eneo hilo la kusini mwa nchi lililoathiriwa na mafuriko ambayo yalisomba kingo za mito na kusababisha vijiji kuzama majini. 
Aidha ametaka kuratibiwa misaada ya dharura haraka iwezekanavyo na kuliagiza jeshi kuwasaidia wale wote walioathirika na mafuriko. 
Nyumba 45,312 zimeathirika na mafuriko nchini Malawi huku idara husika ikiendelea kufanya tathmini kuhusu kiwango cha maafa katika wilaya 14 zilizokumbwa na mafuriko.
parstoday.

Comments