
MFUKO wa dharura wa Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza kutoa msaada wa dola milioni 20 kusaidia waathirika wa kimbunga Idai kilichozikumba Zimbabwe, Malawi na Msumbiji.
Kwa mujibu wa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock mfuko huo wa dharura CERF umetangaza kutenga dola miloni 20 kwa ajili ya kupiga jeki msaada wa kibinadamu kufuatia Kimbunga Idai kilichokumba nchi tatu ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.
Kipaumblele ikitolewa kwa Msumbiji iliyoathirika zaidi na ambayo imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia jana Machi 20 ili kuzika waliopoteza maisha.
Aidha mkuu huyo wa OCHA amesema makundi ya watu walio hatarini wakiwemo watoto, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, watu wanoishi na ulemavu na walio na magonjwa ya muda mrefu ndio watakaopewa kipaumbele.
OCHA imesema fedha hizo pia zitasaidia mashirika ya kibinadmu kuimarisha mipango yao ikiwemo mbinu za kuwasiliana na kuimarisha huduma za maji na huduma za dharura za afya kwa ajili ya kupunguza hatari ya magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji na viini.
Comments