Miaka minane utekelezwaji ilani.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayoshudiwa kila pembe ya Zanzibar, yametokana na utekelezwaji mzuri wa maagizo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Dk. Shein alieleza hayo katika maeneo mbalimbali wakati alipofanya ziara maalum ya kuangalia utekelezwaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 iliyoanza Februari 12 hadi 25 mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka 2015 na chaguzi nyengine, Chama cha Mapinduzi kilinadi ilani iliyoiandaa kwa wananchi ambayo imeainisha utekelezwaji wa mambo mbalimbali ya kimaendeleo kwa jamii endapo chama hicho kitakapopewa ridhaa ya uongozi.
Akizungumza na wana-CCM katika tawi la Mtoni mjini Zanzibar, Dk. Shein, alisema, CCM itahakikisha inatekeleza vyema kila lililoainishwa katika ilani, ili iwe rahisi kwa chama hicho kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Natambua majukumu na wajibu wangu ndani ya chama ikiwemo kusimamia utekelezaji wa sera na ilani ambapo hadi sasa tumeitekeleza kwa kiwango kizuri”, alisema Dk. Shein.
Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein aliwataka viongozi wa chama hicho kuendeleza mshikamano na kuhakikisha wanatumia muda uliobakia hadi kufikia mwaka 2020, ilani hiyo iwe imetekelezwa kwa asilimia 100 katika ngazi zote.
Dk. Shein ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema ili ilani hiyo itekelezwe vyema ni lazima viongozi wa majimbo wahakikishe wanaimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao, hali ambayo itafanikisha utekelezwaji wa ilani bila ya vikwazo.

Comments