
MWAKILISHI wa Jimbo la Mahonda, Balozi Seif Ali Iddi, amesema amefanikiwa kutekeleza ahadi zake nyingi katika fani ya michezo Jimbo la Mahonda, baada ya kutumia shilingi milioni 28,340,000.
Alitoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Jimbo la Mahonda, ulioelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM na Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo hilo katika kipindi cha Mwaka 2015 hadi 2019, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa CCM Mkoa uliopo Mahonda.
Alisema katika kazi ziliofanyika kuinua sekta ya michezo, ndani ya Jimbo hilo, kuna mambo mengi yaliofanyika kuendeleza sekta hiyo.
Alisema amemaua kutumia kiasi hicho cha fedha ikiwa ni hatua ya kuimarisha jamii katika jimbo hilo, ili kusaidia mila na silka njema kwa wananchi wake ikiwa pamoja na kuimarisha afya na kujenga udugu.
“Katika kuufahamu ukweli huo ambapo kipaumbele katika mambo mengi ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda nimeshatekeleza Ilani hiyo kwa kuwaunga mkono wanamichezo wa Jimbo hilo katika kipindi chote cha miaka mitatu iliyopita” alisema Balozi Seif.
Alisema uungaji mkono huo umewawezesha timu mbali mbali za ndani ya Jimbo hilo kupatiwa misaada ya seti za Jazi, Mipira, Fedha za kununulia wachezaji pamoja na kuwahudumia wachezaji wakati wanapokabiliwa na mashindano mbali mbali.
Balozi Seif, aliwapongeza wananchi wa Jimbo hilo kwa kuunga mkono sekta ya michezo kwa kulifanya jimbo hilo kuwa vizuri.
Nae, Mbunge wa Jimbo hilo, Bahati Abeid Nassir, akiwasilisha utekelezaji wa Ilani kwa Mwaka 2017, alisema amefanikiwa kuzimarisha timu ya Mahonda kwa kuipatia shilingi 500,000, timu ya Kazole, shilingi 300,000, timu ya Mwangapwani shilingi 300,000 timu ya Kinduni shilingi 400,000.
Bahati alisema michango hiyo pia aliipatia kikundi cha Karati shilingi 900,000 kwa ajili ya ujenzi wa Ukuta, na vikundi vya Fujoni Changani shilingi 380,000 kwa ajili ya kazi za ushoni.
Comments