
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wakulima wa mwani hasa akina mama kufanya subira huku Serikali yao ikitafuta mwarobaini wa bei ya mwani ikiwa ni pamoja na kujenga kiwanda cha mwani hali ambayo itapaisha bei ya zao hilo hapa nchini.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Kusini Unguja pamoja na kufanya Majumuisho ya ziara yake kwa Wilaya hiyo, yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Residence huko Kizimkazi Mchangamle, Mkoa wa Kusini Unguja ambapo viongozi kadhaa walihudhuria akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein.
Katika hotuba yake hiyo Rais Dk. Shein alisema kuwa anaelewa kuwa bai ya mwani imekuwa ni changamoto kubwa na tokea alipoingua madarakani amekuwa akilifanyia kazi suala hilo lakini mara hii amepata mwarobaini wake.
Alisema kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshafanya mazungumzo na Kampuni kubwa ya mwani ya nchini Indonesia na waameshakubaliana kujenga kiwanda kikubwa cha mwani hapa Zanzibar.
Alisema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya ziara yake aliyoifanya nchini humo mwishoni mwaka jana 2018 ambapo alikutana na viongozi na wafanyabiashara wa zao hilo na kukubaliana kuazisha mashirikiano jambo ambalo linaenda vizuri na hatua iliyobaki ni kusaini Makualiano ya Mashirikiano hivi sasa ili kuanza mchakato.
Alieleza kuwa kufanikisha suala hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupatinda chati zao la mwani katika visiwa vya Zanzibar na kupelekea wakulima wa zao hilo kufainika na kilimo hicho kwani bei ya zao hilo itakuwa juu na kuweza kusaidia kuimarisha pato la wakulima pamoja na pato la serikali.
Aidha, Rais Dk. Shein amewahakikishia wananchi wa Majimbo mawili ya Wilaya hiyo likiwemo Jimbo la Paje na Jimo la Makunduchi kuwa tatizo la uhaba wa maji safi na salama lilo kutafutiwa ufumbuzi na si muda mrefu litakuwa historia.
Aliwataka wananchi wa Michamvi kufanya subira huku juhudi za makusudi zikifanywa na Serikali kupitia Mamlaka yake ya Maji Zanzibar (ZAWA), katika kutatua changamoto wanayoikabili ya uhaba wa maji safi na salama katika kijiji hicho.
Pia, aliwaahidi wananchi wa kijiji cha Mtende Jimbo la Makunduchi kuwa atatekeleza ahadi yale aliyowaahidiya kuwapelekea huduma hiyo muhimu ya maji safi na salama kwa uhakika kutokana na uhaba uliopo wa huduma hiyo.
Rais Dk. Shein pia amekemea uwepo mkuwa wa biashara ya magendo katika ukanda huo na kueleza kuwa licha ya hali hiyo kuwepo na kuanza kupigwa vita tokea uongozi wa Awamu ya Kwanza kutokana na mazingira ya visiwa vya Zanzibar lakini bado imekuwaikitokezea.
Hivyo aliwataka viongozi pamoja na wananchi kushirikiana na Serikali kupitia kikosi chake Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kwani magendo yanaharibu biashara na uchumi wa nchi.
Hata hivyo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kukipongeza kikosi hicho cha (KMKM) kwa kazi nzuri inayofanya katika kupambana na wanaofanya magendo.
Rais Dk. Shein pia, amewataka viongozi wa CCM kwenda kwa wananchi ili kuwasikiliza changamoto zao walizonazosambamba kwenda kutekeleza ahadi walizoziahidi wakati wakiomba uongozi.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuzipongeza taarifa zote mbili zilizotolewa na Wizaya hiyo hiyo ikiwemo ya chama na ya serikali na kueleza kuwa mafanikio ni mengi kuliko changamoto.
Pia, aliipongeza Wilaya hiyo kwa ukusanyaji mzuri wa mapato kwa kuongeza asilimia 30 kutoka mwaka jana ambapo walikusanya jumla ya TZS milioni 369.2 na mwaka huu wamekusanya TZS milioni 488.3.
Rais Dk. Shein pia, alisisitiza suala zima la maadili kwa viongozi wa CCM na kueleza kuwa viongozi wanatakiwa kuwa na nidhamu na kufuata taratibu na miko ya uongozi huku akiwataka Wabunge na Wawakilishi wa chama hicho kutumia lugha nzuri wanapikuwa katika vyombo vyao vya kutunga Sheria ikiwa Barazani ama Bungeni.
Alieleza kuwa Wabunge na Wawakilishi wana haki ya kuiuliza Serikali yao na ni vyema wakapewa majibu ya uhakika na pale inapofikia hatua wanataka kuchunguza jambo lolote basi wachunguze kwa mustakbali wa kuisaidia Serikali kwani huo ndio utaratibu wa vyombo hivyo vya kutunga sheria.
Dk. Shein alisisitiza kuwa hatomstahamilia kiongozi ambaye hana maadili ya uongozi na hafanyi vyema kazi alizopewa kwani kiongozi ni lazima afanye kazi zake vyema kwa kufuata taratibu, seria na kanuni pamoja na Katiba katika kuwatumikia wananchi.
Akielezea suala zima la migogoro ya ardhi, Rais Dk. Shein aliwataka wale wote wanaoshukiwa na utekelezaji wa migogoro wakiwemo baadhi ya viongozi wa serikali kuwacha mara moja kwani inatosha na kuanzia sasa kiongozi yeyote atakaejishirikisha na migogoro hiyo asijekumlaumu.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali Haji Omar Kheir aliwaeleza wananchi wa Wilaya ya Kusini kuwa wako salama na vikosi vyao vyote vinafanya kazi vizuri kikiwemo kikosi cha KMKM.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mussa Ramadhan Haji alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Mamlaka hiyo katika kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi wa Majimbo ya Wilaya hiyo hasa katika kijiji cha Michamvi.
Alieleza kuwa katika bajeti yao ya mwaka huu tayari zimetengwa TZS Bilioni 4 kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji katika Wilaya hiyo kwenye Majimbo ya Paje na Makunduchi na kuwataka wananchi kuvuta subira kwani mchakato unaendelea na si muda mrefu huduma hiyo itapatikana kwa uhakika.
Rais Dk. Shein ameanza ziara yake katika Kisiwa cha Pemba hivi leo ambapo anatarajiwa kufungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya Serikali kisiwanihumu ikiwa nipamoja na kuzungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya zote za Pemba.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Comments