Serikali yataka ushirikiano kudhibiti saratani..

NAIBU Waziri wa Afya, Harusi Said Suleiman, amesema, kuna ongezeko la maradhi ya yasiyoambukiza ikiwemo saratani, hivyo, jitihada zaidi zinahitajika kuielimisha jamii kujikinga na maradhi hayo.
Hayo aliyaeleza katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani katika hafla iliyofanyika Kwa Binti Hamrani wilaya ya Mjini Unguja jana.
Alisema, kwa mujibu wa takwimu zilizopo hospitali ya Mnazimmoja ambazo zimejumuisha wagonjwa waliofika hapo, idadi imekuwa ikiongezeka katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2017.
Alisema, mwaka 2015 waligundulika wagonjwa 271 huku mwaka 2016 ikiwa na wagonjwa 392 na mwaka 2017 wagonjwa 560.
Alisema, idadi hiyo ni kubwa na yenye kutisha  huku saratani ya shingo ya kizazi, matiti na tenzi dume  zikiongoza.
Alisma,  kati ya wagonjwa wanaogundulika  na maradhi hayo, kwa asilimia kubwa wanafika hospitalini ikiwa ugonjw upo katika hatua kubwa, hali ambayo  hupelekea kuongezeka kwa gharama  za matibabu.
“Lakini hata athari zitokanazo na maradhi haya zinakuwa kubwa”, alisema.
Alisema, vifo vingi  vinavyotokana na maradhi hayo husababishwa na  kukosa au  kuwa na uelewa mdogo  wa namna ya kujikinga, njia za  kufuata ili  kuyagundua  mapema na kupata tiba sahihi.
Hata hivyo, Naibu Waziri, alisema, hadi sasa hakuna daftari maalum la kuwekea takwimu za maradhi hayo, lakini, jitihada  zimeanza kuchukuliwa  za kuandaa daftari hilo ambapo  wafanyakazi wawili  wameshapatiwa mafunzo hayo.
“Hivi karibuni wafanyakazi wengine zaidi watapatiwa taaluma hiyo na mara baada ya kumalizika mafunzo mfumo wa ukusanyaji data za saratani utaanzishwa,” alisema.
Hivyo, aliitaka jumuiya ya wagonjwa wanaoishi na saratani kuendeleza jitihada zao za kuelimisha jamii juu ya kujikinga na maradhi ya saratani na kufanya uchunguzi  wa afya ili kugundua mapema na kupatiwa tiba sahihi.
Alisema, jitihada kubwa zilizochukuliwa na wizara  ni kuanzisha  kitengo cha maradhi yasiyoambukiza ,kusomesha wafanyakazi wa afya akiwemo daktari bingwa  wa uchunguzi  wa maradhi ya saratani, na daktari bingwa wawili  wa tiba za saratani ambao wanaendelea kufanyakazi  katika kitengo cha tiba za saratani hospitali ya Mnazimmoja.
Zanzibarleo.

Comments