
NAIBU Waziri wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Lulu Msham Abdalla, amesema, wizara hiyo imeandaa mikakati ya kifedha kwa ajili ya matayarisho ya timu zitakazoshiriki kimataifa ili kukabiliana na mashindano hayo kwa uhakika na kupata ushindi.
Aliyasema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi huko Chukwani wakati akijibu swali aliloulizwa na Mwakilishi wa Chake Chake, Suleiman Sarahan Said, aliyetaka kujua wizara hiyo imejipangaje kwa timu zinazowakilisha kimataifa na kurejea na ushindi.
Alisema katika kuhakikisha timu zinakwenda kushindana na zinarudi na ushindi, hivi sasa tayari matayarisho ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, yanaendelea huku mikakati kabambe ikiandaliwa.
Alieleza kuwa vijana hao wakiongozwa na kocha mkuu, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wameteua vijana 30 na wanatarajiwa kuanza mazoezi nje ya kambi kila wiki kwa siku za Jumamosi na Jumapili.
“Nakubali kuwa Zanzibar inashiriki katika michezo ya kimataifa hasa mchezo wa mpira wa miguu yakiwemo mashindano yaliyoandaliwa na CECAFA na CAF, na ni kweli kuwa mwaka uliopita ulikuwa na misukosuko mengi kwa timu zetu kama tulivyoshuhudia”, alisema.
Hata hivyo, alisema, tatizo kubwa lililoonekana ni kuwepo kwa katiba ambayo haikidhi haja na kuwepo kwa viongozi wasiokuwa madhubuti.
Pia, alisema, wizara imetafakari kwa kina juu ya matatizo yaliyojitokeza mwaka jana na kujipanga kuhakikisha kuwa hayatatokea tena kwa kuanzia na ZFA kuifanyia mapitio katiba ya mwaka 2010 na badae kufanyika zoezi la kufanya mapitio ya katiba za vyama vya michezo katika ngazi zote.
Waziri Lulu, alisema, vyama hivyo vya soka vitafanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba hizo mpya ambapo wizara inaamini vitakuja na viongozi wenye uwezo na wenye nia ya kusimamia na kuuendeleza mchezo huo.
Alieleza, Zanzibar inashiriki mashindano ya mchezo wa mpira wa miguu yanayoandaliwa na CECAFA ikiwemo ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20 pamoja na ile ya wanawake na wanaume kwa wakubwa, hivyo, lazima kuwepo mikakati itakayosaidia kupata matokeo bora kwenye michuano hiyo.
Zanzibarleo.
Comments