JAJI mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu amesema taasisi za umma zinathamini mchango mkubwa wa serikali katika kufanikisha mageuzi ya kiutendaji, ili kufanikisha dhana ya utoaji bora wa haki katika jamii.
Amesema taasisi hizo, ikiwemo mahakama, Ofisi ya Mwendesha mashtaka, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, zinaridhishwa na juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha miundombinu, upatikanaji wa vifaa na mafunzo kwa watendaji.
Jaji mkuu alisema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, wakati akitoa nasaha katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Sheria Zanzibar.
Alisema kutokana na mchango huo shughuli za Mahakama zimeimarika, hususan baada ya Serikali kuteuwa majaji, mahakimu na makadhi wapya katika ngazi zote za mahakama Unguja na Pemba.
Alisema kwa nyakati tofauti watendaji wa taasisi hizo wamepata mafunzo ya ndani na nje ya nchi, hivyo kujenga uwezo katika kufanikisha dhana ya serikali ya upatikanaji wa haki bora kwa jamii.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuimarisha mhimili huo wa dola (mahakama) kimuundo na kibajeti, sambamba na hatua ya kuanzisha mfuko wa mahakama, ambao utaiwezesha taasisi hiyo kufanyakazi zake kwa ufanisi zaidi.
Jaji Othman aliipongeza serikali kwa kuanzisha mradi wa usalama na kufunga kamera za CCTV, hatua itakayosaidia sana kuimarisha usalama wa mji na kubaini makosa mbalimbali, yakiwemo ya usalama barabarani, hivyo kuipunguzia kazi mahakama
Jaji Othaman, alipongeza azma ya serikali ya kuanzisha ujenzi wa jengo jipya la mahakama kuu katika eneo la Tunguu, litakaloambatana na skuli ya mafunzo ya sheria ‘Law school’.
Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Said alisema uimarishaji wa taasisi za umma utarahisisha upatikanaji wa haki katika suala zima la Utawala Bora.
Alisema changamoto iliyopo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za umma, inatokana na ukosefu wa utaalamu, weledi na ukiukwaji wa maadili.
Alisema kuna umuhimu wa kuimarisha mfumo ili kuwajengea zaidi uwezo watendaji wa taasisi hizo ili hatimae waweze kufanyakazi zao kwa ufanisi.
Mapema, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee alisema utatuzi wa migogogro kupitia mifumo isiyo rasmi, hususan ule wa kujichukulia sheria mikononi ina madhara makubwa kwa jamii.
Alisema Ofisi ya DPP itaendelea kushirikiana na taasisi nyengine za umma, ili kufanikisha dhana ya upatikanaji wa haki, ili jamii iweze kupata haki kwa usawa.
Zanzibarleo
Comments