Dk. Shein ahimiza utawala wa sheria.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema umadhubuti wa nchi unategemea kwa kiasi kikubwa nchi ilivyojidhatiti katika kudumisha utawala wa sheria.
Aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya siku ya sheria Zanzibar yaliyofanyika huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete Pemba.
Dk. Shein alisema maadhimisho ya siku ya sheria yana umuhimu hasa katika kutoa mwamko kwa wananchi katika kuzifahamu na kuzitii sheria za nchi zikiwa ndio msingi wa kukuza utulivu, amani na maendeleo.
Aliongeza kuwa suala la kuzifahamu na kuzitii sheria husaidia jamii kuishi kwa nidhamu na kuheshimiana katika maisha ya kila siku, kwani sheria lazima zitambuliwe ili wananchi waweze kupambanua haki na wajibu.
Alisema ikiwa jamii itaishi bila ya kufuata sheria basi utakosekana ustaarabu katika utekelezaji wa mambo kwani sheria ni suala nyeti linalogusa maisha katika nyanja mbali mbali.
Alisema kwa msingi huo mamlaka tatu zilizopo katika mfumo wa mgawanyo wa madaraka yaani serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama ni lazima zihakikishe zinashikamana bila ya kuathiri uhuru wa sehemu moja.
Aliwahimiza wananchi kuendelea kutii sheria za nchi kama katiba inavyoelekeza huku akiwahimiza viongozi wa dini nchini kuendelea kuhubiri utii wa sheria za nchi.
Alieleza kufurahishwa na kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Uimarishaji wa Taasisi za Umma ni Ustawi Bora wa Upatikanaji wa Haki kwa Jamii” na kusisitiza kuwa kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha taasisi za umma kwa maendeleo ya jamii.
Alisema serikali ya Mapinduzi katika awamu zote saba imefanya jitihada kubwa kuimarisha taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa ustawi wa upatikanaji wa haki kwa jamii unakuwa wa uhakika.
Dk. Shein alieleza jitihada zinazochukuliwa na taasisi zinazosimamia haki na sheria zinazozingatia maendeleo ya ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu ya mwaka 2015-2020 ambayo katika ibara ya 145 inafahamisha jinsi ya kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa ufanya maboresho katika utendaji wa vyombo vya maamuzi ikiwemo mahkama, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Pamoja na hayo, alieleza hatua zilizochukuwa na serikali katika matengenezo ya majengo ya Mahkama huku akieleza kuwa serikali imo mbioni kujenga jengo la Mahkama Kuu mpya pamoja na jengo la skuli ya sheria (law school), Tunguu ambapo jumla ya shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa kazi hiyo.

Comments