Wakizungumza na Zanzibar Leo, baadhi ya wananchi na wafanyabiashara
waliopo katika maonyesho hayo yanayofanyika Maisara, ikiwa ni
shamrashamra za miaka 55 ya mapinduzi, walisema ipo haja ya kuwekwa
vifaa vya kupozea hewa (misting system) kama zinavyofanya nchi nyengine
ili kupunguza joto kali liliopo eneo hilo.
Mmoja ya wananchi hao, Hamad Mohammed Haji, alisema ikiwa wizara
itaweka vifaa hivyo, watavutia wananchi wengi zaidi kwa sababu eneo hilo
lina joto kali.
Aidha alisema kama wizara itashindwa kuweka kifaa hicho basi inaweza
kuweka ‘misting fans’ ambazo zina uwezo mkubwa wa kupoza hewa tofauti na
feni za kawaida.
“Kwa kweli joto kali sana hasa kipindi hichi cha Januari ambacho
maonyesho haya huwa yanafanyika, tunajua wizara yetu ni sikivu na
inaweza kutuwekea mazingira mazuri sisi wafanyabiashara ili kuwapa fursa
wananchi kutembelea na kupata elimu katika tasisi mbalimbali zilizopo
hapa,” alisema.
Kwa upande wake, Khadija Khamis Ali, alisema joto linawakoshesha fursa wananchi kutembelea mabada hayo.
“Kwa kweli katika banda letu tulitembelewa na Rais mstaafu wa awamu
ya sita, Dk. Amani Abeid Karume, lakini alishindwa kukaa kutokana na
joto lililokuwepo na hata wananchi wengine wanaotembelea huwa hawakai
kupata elimu kutokana na joto,” alisema.
Hivyo walitumia fursa hiyo kuiomba wizara kulifanyia kazi suala hilo ili maonyesho yajayo yawe bora zaidi.
Katika hatua nyengine, waliiomba wizara kuchanganya mfumo wa kuweka
wafanyabiashara na taasisi za serikali hatua ambayo itawawezesha
mwananchi kutembea na kupata elimu, badala ya mfumo wa sasa ambapo
mabanda ya taasisi za serikali yamewekwa pamoja.
Comments