Wanafunzi Karume walilia usajili NACTE.

WANAFUNZI wanaosoma Chuo cha Karume Institute of Science and Technology Mbweni, wameiomba wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuingilia kati suala la kutopatiwa usajili na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Zaidi ya wanafunzi 100 wanaosoma katika Chuo hicho hasa kada ya ufundi wa maabara ‘Laboratory Technician’.
Wakizungumza na Zanzibar Leo huko Mbweni, baadhi ya wanafunzi hao walisema kitendo cha kukoseshwa usajili kimewaathiri sana kisaikolojia na kuwavunjia malengo yao waliojiwekea.
Aidha walisema jambo hilo wameanza kulifatilia tangu wakiwa mwaka wa kwanza wa masomo (2016), ambapo hadi sasa hawajapata majibu sahihi juu ya na suluhisho la kupwatiwa usajili.
Walisema, wanaamini hakuna tatizo linalowafanya kutosajiliwa kwani kwa mujibu wa vigezo vilivyotakiwa na chuo wakati walipoomba kujiunga walivitimiza.
Kauthar Yussuf ni mwanafunzi wa chuo hicho ambae yupo mwaka wa tatu, alisema pamoja na kufuatilia ngazi zote bado hawajapata majibu kutoka kwa uongozi wa chuo hicho.
Aidha alisema wakati wanaomba kujiunga na kada hiyo walitakiwa kuwa na alama ya ufaulu wa D nne, lakini cha kushangaza hivi karibuni wanaambiwa hawapati usajili hadi wawe na alama ya ufaulu wa D tano kwa mujibu wa mtaala wa Arusha ambao waliufata.
Nae, Mwanafunzi Silima Ali Mashauri, alisema hawakuingia chuoni hapo kimabavu, bali waliingia kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na chuo hicho.
Aidha alisema kama hawana vigezo vya kusajiliwa basi walikuwa waambiwe mapema kuliko kupoteza muda na fedha walizokuwa wakichangia.
Abdalla Faki Ali ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, alisema ni dhahiri kuwa uongozi wa chuo umeshindwa kulitatua tatizo hilo na kuendelea kuwaweka njia panda bila ya kupata suluhisho.
Kwa upande wake rais wa serikali ya wanafunzi Chuo cha Karume, Hakim Abdulla Mohammed, alisema tatizo hilo tayari ameshaliwasilisha rasmi katika uongozi wa chuo.
Zanzibaleo.

Comments