Ujenzi madaraja ya kisasa kuimarisha uchumi.

WIZARA ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, imesema serikali itahakikisha madaraja na mitaro inayojengwa inakuwa na ubora unaotakiwa ili idumu kwa muda mrefu.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mohammed Ahmada Salum, alisema hayo alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa madaraja ya Kibondemzungu, Mwanakwerekwe na mtaro wa Kiembesamaki.

Alisema ili kuhakikisha ujenzi huo unakuwa katika viwango, wanafanya ziara za mara kwa mara katika maeneo hayo ili kuzungumza na wakandarasi wanaojenga miundombinu hiyo.

Alisema serikali inafanya kila jitihada kuondosha usumbufu na kuwarahisishia usafiri wananchi.
Alisema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutachochea mipango ya serikali katika kutekeleza sera ya ukuaji wa uchumi.

“Ujenzi wa miundombinu hii ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2015-2020, ambayo Dk. Shein anaisimamia,” alisema.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa madaraja hayo ni chachu ya kuondosha changamoto zote zilizokuwa zikitokea kipindi cha mvua kwa wananchi kupoteza maisha na miundombinu ya barabara kuharibika.

Mhandisi Nassor Ramadhan, ambaye ni mkuu wa ujenzi wa madaraja hayo, alisema ujenzi huo umetekelezwa kwa asilimia 30, hivyo alitumia fursa hiyo kuiomba jamii kuwa wastahamilivu kwani matarajio yao ndani ya mwezi wa Machi kazi itakuwa imekamilika.

Daraja la Kibondemzungu linayojengwa na kampuni ya MECCO, unatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu na utagharimu kiasi ya shilingi bilioni 4.8.

Comments