Soud aguswa utekelezaji ilani CCM.

WAZIRI asiekuwa na wizara maalumu, Said Soud Said, amesema jinsi CCM inavyotekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa vitendo, kwa kuwafikishia huduma wananchi bila ya ubaguzi, hakuna chama chengine cha siasa kinachoweza kushinda uchaguzi.

Alisema katika miaka hii 55 ya mapinduzi ya Zanzibar, wananchi wa Unguja na Pemba, wamefikiwa na huduma za lazima, ikiwemo matibabu, huduma ya maji safi na salama, barabara na elimu, yaliotekelezwa kupitia ilani ya CCM bila ya ubaguzi.

Alisema hayo Mjiweni Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, baada ya kufungua mradi wa maji safi na salama, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za miaka 55 ya mapinduzi Zanzibar, ambapo kilele chake kitafanyika Pemba Januari 12, mwaka huu.

Alisema CCM, sio tu imewafikishia huduma wananchi wote, lakini imesimamia kwa kiasi kikubwa, umoja, mshikamano, amani na utulivu na kuwafanya wananchi kuishi kwa upendo.

Alisema mfano wa maendeleo yaliosimamiwa na CCM na hasa baada ya kufanyika kwa mapinduzi ya Zanzibar, ni ufunguzi wa mradi huo wa maji safi na salama, ambapo utawanufaisha wananchi wa Mjiweni na vijiji jirani.

Kuhusu mradi huo wa maji safi na salama, aliwataka wananchi kuhakikisha wanautunza sambamba na kuchangia huduma za maji kwa wakati, ili ZAWA iweze kufanya matengenezo inapotokezea hitilafu.

Alisema hakuna mwananchi alie na uwezo wa kulipia huduma ya maji, elimu wala matibabu ndio sababu serikali ikaamua kuweka huduma hizo bila ya malipo.

Aidha aliwataka vijana na wazee kuendelea kuyaenzi na kuyalinda mapinduzi ya Zanzibar kwani yamekuwa ndio dira ya kuwafikishia maendeleo na upendo wazanzibari.

Alieleza kuwa, kabla ya mapinduzi wananchi waliokuwa wakijishughulisha na kilimo, walilazimika kulipa kodi za ardhi kwa watalawala na kubakiwa na kipato kidogo, baada ya mavuno.

“Leo kila mmoja anafanya shughuli zake iwe ni ufugaji, uvuvi au kilimo bila ya kulipia ardhi na anachokipata ni kwa ajili yake na familia yake,”alieleza.

Zanzibarleo.

Comments