Dk. Shein aliyasema hayo jana katika hafla ya uzinduzi wa uwanja wa
Mao Tse Tung uliopo Kikwajuni Mkoa wa Mjini Magharibi, ambao umejengwa
kwa msaada wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa mashirikiano ya
pamoja na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema michezo ni jambo la ridhaa na maelewano, hivyo matatizo yote
yanayojitokeza, ni lazima yashughulikiwe na kumalizwa kwa busara.
Alitoa indhari kwa kubainisha kuwa kuanzia sasa hatokuwa tayari
kusaidia shughuli za kimichezo, ikiwemo soka endapo tabia ya kupeleka
kesi hizo mahakamani itaendelea.
“Acheni tabia hiyo, mnaitia aibu nchi yetu, nataka nikwambieni kuwa
FIFA inatuonea imani tu juu ya jambo hilo, ni matumaini yangu kuwa kesi
za michezo hazitafikishwa tena mahakamani” alisema.
Aidha, Dk. Shein alisema serikali inakusudia kuongeza bajeti ya
Wizara ya Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia mwaka ujao wa
fedha, ili kuimarisha na kuendeleeza michezo mbali mbali nchini.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na uimarishaji wa timu ya Taifa
ya mpira wa miguu, ili kuleta ushindani na kuwa miongoni mwa timu bora
katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Dk. Shein alieleza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itahakikisha inafanikisha azma yake ya kujenga uwanja mkubwa wa kisasa
utakaochukua watu 45,000 kutoka maeneo yaliyotengwa huko Fumba pamoja na
Tunguu.
Katika hatua nyengine Dk. Shein aliigiza Wizara ya
Vijana,Utamaduni,Sanaa na michezo kuandaa programu nzuri itakayowezesha
matumizi bora ya kiwanja hicho, ili uweze kudumu.
Alisema ni vyema kukawepo utaratibu wa kuweka viingilio katika
baadhi ya mashindano ili kuweza kupata fedha zitakazowezesha kukifanyia
matengenzo madogo madogo kiwanja hicho pale panapohitajika.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ujenzi wa uwanja huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Nae Waziri wa Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Balozi
Ali Abeid Karume alitoa shukurani na pongezi kwa Dk. Shein kwa jitihada
zake za kuhakikisha uwanja huo unajengwa upya na una kuwa wa kisasa.
Balozi Karume alimponmgeza Dk. Shein kwa kuweka kipaumbele suala la
kuimarisha michezo, hivyo, akaahidi Wizara yake kuwaendeleza vijana
pamoja na kukitunza ipasavyo kiwanja hicho.
Aidha, Balozi Karume alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio na matunda ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Nae Balozi Mdogo wa China anaefanya kazi zake hapa Zanzibar Xie
Xiuowu alisema ujio wa mradi huo utaendeleza uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya China na Zanzibar.
Aidha, alisema kukamilika kwa kiwanja hicho pamoja na ujenzi wa
viwanja mbali mbali vya michezo ya ndani (indoor games) kutaimarisha
viwango vya wanamichezo wa Zanzibar na hivyo kufanya vyema katika
mashindano mbali mbali.
Zanzibarleo.
Comments