Dr. Shein awekajiwela msingi katika jengo jipya la ZURA.

Image may contain: one or more people, people standing, beard and outdoorRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yamefanywa kwa lengo la kuleta mabadiliko, uhuru, ukombozi pamoja na kujenga misingi ya usawa umoja na heshima kwa Wazanzibari wote.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kuweka jiwe la msingi jengo jipya la Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) linalojengwa sambamba na Ofisi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja na ZURA huko Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduizi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliyojenga utu wa Wazanzibari na bado yanaendelea kuifanya Zanzibar iweze kuimarika na kupendwa duniani kote.

“Mapinduzi yameleta heshima na mabadiliko makubwa ndio maana tunasema Mapinduzi Daima, kwani leo ni miaka 55 tokea Zanzibar iwe huru”,alisisitiza Dk. Shein.

Alieleza kuwa katika miaka 55 Zanzibar imefanya mambo makubwa sana ambayo wakoloni hawakuyafanya lakini mara tu baada ya Mapinduzi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kuyafanya na kuleta mabadiliko makubwa.

Dk. Shein alieleza umuhimu wa maji kwa mwanaadamu ambayo huduma hiyo inadhibitiwa na mamlaka hiyo na kusisitiza kuwa bila ya maji mwanaadamu hawezi kuishi na hakuna kiumbe hata mmoja ambae anaweza kuishi bila ya kuwepo kwa huduma hiyo muhimu.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa ni vyema kukawekwa nidhamu ya matumizi ya maji na ndio maana Serikali zote duniani zinaanzanisha na kuwezaka Taasisi za udhibiti na ndio maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwezi April mwaka, 2015 ikaunda Taasisi hiyo.

“Mwanzo ilipoundwa Taasisi hii haikufahamika vyema madhumini yake lakini mara baada ya watu kujua basi kila mmoja alitaka kufanya kazi ZURA na wanasema Kule Mambo yamenoga kwani mwanzo haikuwa hivyo watu walidharau” alisisistiza Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa chombo cha udhibiti katika Serikali ni muhimu sana na hatua hiyo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuanzisha Taasisi hiyo ambayo pia imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika zoezi la utafutaji wa Mafuta na Gesi hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo hilo kutasaidia kwa kuwaweka wafanyakaazi wa Wizara hiyo na Taasisi zake pamoja na kupelekea kufanya kazi vyema.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kwa kueleza kuwa Maktaba iliopo hivi sasa ambayo iko jirani na jengo hilo la ZURA itavunjwa NA kujengwa mpya tena ya kisasa mara baada ya kumaliza jengo hilo jipya kupitia mwamvuli wa ZURA.


Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa kamwe neema ya MwenyeziMungu hazibezwi, hazizarauliwi na badala yake zinatunzwa na ujenzi wa jengo hilo ni neema za Mapinduzi hivyo, lazima litunzwe.

Aidha, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Ardi, Nyumba, Maji na Nishati kupitia ZURA kulikarabati jengo lake Wizara linalotumika hivi sasa mara baada ya kuhama ili liweze kupendeza na kusaidia kwa mambo mengine.

Aliiambia Bodi ya ZURA kufanya kazi ya kuwafundisha wafanyakazi wenye uwezo kwa kuwapatia mafunzo ili wabobee kwenye taaluma kwani Serikali inahitaji wataalamu ambao watatoka miongoni mwao wa fani zote ambao ZURA itawahitajia.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mara baada ya kukamilika kwa jengo hilo ambalo tayari ofisi hiyo mara baada ya kukamilika ni vyema wafanyakazi wa ZURA wakafanya kazi za nje kwani ujenzi huo utatekeleza haja na hoja ya wafanyakazi kufanya kazi zao vyema.

Rais Dk. Shein aliitaka Bodi ya ZURA kutojisahau na kuitaka kufuata Sheria ya ZURA na utumishi wa Umma ya Namba mbili ya mwaka 2011 kwani ndio nyenzo muhimu ya kuongoza ZURA na wasiende nje zaidi ya hapo.

Alisema kuwa yeye hana tatizo na Bodi iwapo itatoa tunza fulani kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo wanapofanya vizuri, ila jambo la muhimu ni kufuata Sheria na Utaratibu ikiwa ni pamoja na kumshirikisha Waziri husika wa Wizara hiyo.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa Bodi inapotaka kupandidha mishahara ni vyema iseme na imueleze Waziri na sivyo kama ilivyofanywa na baadhi ya Bodi ambazo zimechukua madaraka yasio yao na kufanya makosa makubwa.

Alisema kuwa Bodi zinafanya kazi kupitia kwa Waziri, na Sheria hizo zipo lakini walikuwa hawashauriani na ndio maana marekebisho yanataka kufanya lakini kunakuwa na changamoto kutokana na hali.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa sheria zipo kanuni zipo na kusisitiza kuwepo haja ya kuwajibika na kuitumia fursa hiyo kukumbusha kuwa kazi iliyopo ni moja ambayo ni kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Alisema kuwa yeye pamoja na viongozi wengine waliochanguliwa na wananchi ni vyema wakawatumikia wananchi na kufanya kazi kwa pamoja kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mambo yake mazuri licha ya kuwepo wachache wanaoikejeli.

Alisisitiza kuwa katika nchi za Afrika Mashariki Zanzibar pekee ndiyo uchumi wake umeweza kuimarika na kukua kwa asilimia 7.7 mnamo mwaka 2018. 

Alieleza kushwangazwa kwake na wale waliosema kuwa uchumi wa Zanzibar unaanguka na uko chini lakini hakuwajibu na kama ilivyo kawaida yake yeye hujibu kwa vitendo.

Aliongeza kuwa licha ya uchumi mdogo wa Zanzibar lakini bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendesha elimu na afya bure.

Alieleza kuwa jengo hilo linajengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zipatazo Bilioni 20 ambazo zinatokana na uchumi wa Zanzibar pamoja na miradi mengine kadhaa inayoendelea kutekelezwa kutokana na uchumi huo huo wa Zanzibar.

Alieleza kuwa kutokana na mafanikio mbali mbali yaliopatikana Zanzibar pia, kuna nchi zinakuja kujifunza Zanzibar na kutoa mfano wa Pencheni jamii kwa wazee na kueleza kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni nchi mbili tu ambazo zinatekeleza Pencheni hiyo na ipo moja ambayo inajikongoja.


Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara pamoja na ZURA kwa jambo hilo la ujenzi wa jengo hilo na kuwasisiatiza kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano hatua ambayo itaimarisha na kuleta manufaa zaidi na mafanikio kwa jumla. 

Nae Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib alieleza kuwa juhudi kubwa busara na hekima alizozichukua Rais Dk. Shein ndizo zilizochangia kuimarika kwa ujenzia wa jingo hilo na kumpongeza kwa miongozo aliyoitoa katika kuhakikisha jengo hilo linajengwa tena kwa kiwango cha hali ya juu.

Waziri Salama alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa wafanyakazi wa Wizara yake kwa kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanaitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisema kuwa wafanyakazi wa Wizara yake wamekuwa wakifanya kazi kwa mashirikiano makubwa miongoni mwao kati yao Wizara, Bodi pamoja na Idara zake zote na kueleza kuwa anaamini kuwa iwapo malighafi zote zinazohitajika zitapatikana basi kabla ya kumaliza muda wake Rais Dk. Shein atalizindua jingo hilo.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Alhalil Mirza alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni utekeleza Malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020 pamoja na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Aidha, alisema kukamilika kwa aujenzi huo kutaondosha changamoto ya eneo la kufanyia kazi kwa taasisi hiyo ya ZURA.

Alieleza kuwa Kampuni ya HAINAN International ya China ilikidhi vigezo vilivyotakiwa na kukubali kuanza kazi za ujenzi ambapo gharama zote za ujenzi huo zinagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hadi kumalizika kwake jumla ya TSh Bilioni 20.2 zinatarajiwa kutumika.
Alisema kuwa muda wa ujenzi kwa mujibu wa mkataba ni miaka miwili kuanzia Februari 2, 2018 hadi Februari 2020 kwa kufanikisha mambo yote ya msingi ikiwemo kujenga majengo mawili ya ghorofa ambayo yatakuwa na sehemu ya chini ya ardhi kwa ajili ya kuegesha magari 50.

Sehemu nyengine ni ghorofa moja ya chini, ghorofa saba za kwenda juu, lifti mbili, ujenzi ambao utakuwa kwa zege kwa ghorofa zote pamoja na kuwekwa vifaa vya usalama, vifaa vya umeme na maji, kupaka rangi na kutengeneza mandhari ya nje pamoja na bustani kwa mujibu wa mchoro.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo makamo wa Piliwa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, ambapo kabla ya kuweka jiwe hilo la msingi alitembelea ujenzi huo na kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa Wizara pamoja na viongozi wa Kampuni ya HAINAN International ya China.Image may contain: outdoorImage may contain: 7 people, people smiling, people standing and suitImage may contain: 10 people

Comments