Watu
wawili wamefariki dunia mkoani Kagera katika matukio mawili tofauti,
likiwamo la mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Laurian Kakoto (80),
mkazi wa kijiji cha Ihunga kata Kishanda wilayani Muleba, kukatwa sehemu
zake za siri na wahusika kuondoka nazo.
Akizungumza
na waandishi wa habari, kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus
Malimi amesema kuwa baba huyo aliondoka nyumbani Januari 7 mwaka huu
kwenda kuhemea lakini hakurudi hadi maiti yake ilipogunduliwa na
wananchi ikiwa imezikwa huku nyayo za miguu zikiwa zinaonekana juu ya
kaburi, Januari 08 saa moja asubuhi.
Kamanda
Malimi amesema kuwa baada ya wananchi kugundua tukio hilo walitoa
taarifa polisi, ambapo walifika na kufukua mwili huo uliokuwa umezikwa
kwa kutanguliza kichwa chini, na kukuta amekatwa kwa kitu chenye ncha
kali shingoni na sehemu za siri.
Aidha
kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wananchi
waliojichukuliwa sheria mkononi kwa kuchoma moto nyumba 16 na kufyeka
migomba, mali za watu waliowatuhumu kumuua mwendesha bodaboda mmoja
Albert Antipas, aliyetoweka tangu Januari 02 mwaka huu na maiti yake
kupatikana ikiwa katika bwawa la kufugia samaki, Januari 07.
Amesema
kuwa maiti ya mwendesha bodaboda huyo ilikutwa ikiwa imefungwa kwa
kamba mikononi na miguuni, na kisha kufungwa katika jiwe na kuzamishwa
katika bwawa hilo.
Baada
ya wananchi wa kijiji cha Kibingo tarafa ya Murongo wilayani Kyerwa
kusikia kuwa watuhumiwa wamekamatwa na polisi, ndipo walipokwenda
kuchoma moto nyumba zao.
Comments