Mitihani ya marudio kidato cha pili Januari 14.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imesema mitihani ya marudio ya kidato cha pili itafanyika kuanzia Januari 14 mwaka huu na kumalizika Januari 22 kwa wanafunzi wa skuli za serikali na binafsi.
Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo (taaluma) Madina Mjaka Mwinyi, aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, ofisni kwake Mazizini.
Mitihani hiyo itafanyika baada ya kufutwa kwa mitihani ya awali kutokana na kubainika imevuja na kuangukia mikononi mwa  watu wasiohusika.
Aliwataka walimu wakuu kufanya maandalizi ili kuwezesha kufanyika kwa mitihani hiyo katika mazingira salama.
Aliwashukuru walimu kwa kuendelea kufundisha na kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha pili wanaendelea kuhudhuria madarasani.
Aliwashukuru wazazi, jamii kwa kuwa watulivu na kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa watulivu katika kipindi ambacho mitihani ilisitishwa.
Alisema katika kipindi cha mitihani ya marudio, wanafunzi wasiofanya mitihani na wananchi hawatakiwi kuonekana katika maeneo ya skuli wakati mitihani ikiendelea.
Pia alisema wizara imezuwia kambi za aina yoyote zinazohusiana na mitihani kuanzia Januari 7, 2018.

Comments