Mbunge CHADEMA Amwangukia Rais Magufuli Kuhusu Korosho.

Ndugu wanahabari nawatumia taarifa hii, kwa nia ya kufikisha kilio cha wakulima wa korosho kwa *Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk,John Pombe Magufuli* kwasababu ndio zao tegemeo la kiuchumi kwa sasa.

Kama mnavyojua mkoa wa Mtwara umekuwa ukiongoza kwa kuzalisha korosho nyingi ikifuatiwa na mkoa wa Lindi,Ruvuma na Pwani pamoja na mikoa mingine mipya ambayo inaongezeka siku hadi siku.

Mtakumbuka baada ya mvutano kati ya serikali na wafanya biashara (wanunuzi wa korosho) baadae serikali iliamua kutangaza kuzinunua korosho zote kwa Tsh.3,300/-kwa kilo.

Zoezi hili lilifanyika kwa maamuzi ya haraka kabla ya kupata ushauri wa kitaalamu lakini pia utafiti wa kina wa namna ya kufanikisha zoezi hili la ununuzi wa korosho ikiwa ni pamoja na kupata uhakika wa soko la korosho na taratibu zingine.

Hata hivyo, itakumbukwa wakati huo wanunuzi na makundi yao walishauri namna bora ya kutekeleza maelekezo hayo bila mafanikio.
 
Wakati wa kikao cha mashauriano cha Mkoa wa Mtwara (RCC) tulipokea taarifa kwamba kwa mwaka  nchi ina uwezo wa kubangua tani 20,000 tu kati tani 270,000 zinazotarajiwa kukusanywa.

Taarifa hii inapingana na taarifa ya Waziri wa viwanda  kwamba tani 100,000 zitabanguliwa na hivyo serikali sasa inatafuta wadau ili wawezi kununua ziada ya tani 150,000.

Hivyo ndugu wanahabari, nawaanfikia leo ili kutoa mrejesho wa yanayoendelea katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kwa wakulima baada ya kufanya uchunguzi wangu binafsi kama *Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Ndanda* ambao na wao wako katika Kilio cha kutolipwa.

Ifahamike kwamba, baadhi ya wakulima wanalipwa, wale wanaizalisha zaidi ya tani 1.5 wao hawalipwi, wakiwemo makundi ya *Wazee, wajane na warithi* Ivi kuwaongezea uchungu wa maisha kwa kisingizio cha uhakiki,

*Yafuatayo ni matatizo yaliyopo kwenye tasnia ya Korosho kwa sasa*

1. Utaratibu wa malipo umekuwa wa kusuasua sana tofauti na taarifa alizopewa *Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu*

2. Wakati kinachodaiwa kuwa zoezi la *uhakiki* kikiendelea kuna *viashiria vya rushwa* kutoka kwa wahakiki.

3. Wakulima wamegawanywa kwa makundi makundi na hivyo kuwafanya wawe wanyonge zaidi

4. Taarifa za malipo zimekuwa za siri kiasi kwamba  hata viongozi wa vyama vya msingi hawana taarifa wala kufahamu kinachoendelea juu ya wakulima waliokusanya korosho maghalani, ivyo kuhatarisha uhai wa vyama ambavyo vitakumbwa na madeni makubwa, yakiwemo ya wabebaji na wasafirishaji.

5. Matumizi makubwa ya nguvu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, jambo hili liko maeneo mengi, kubwa zaidi ni tukio lililotokea Nachingwea, viongozi wa vyama vya msingi wamepigwa na wanajeshi kwa kushirikiana na polisi ofisini kwa Katibu tawala (DAS), ushahidi upo na waliofanya tukio hilo wanafahamika kwa majina

6. Uwezo mdogo wa wahakiki na ujuzi kuhusiana na zao la korosho, wahakiki nao wako mafunzoni, badala ya kutekeleza wajibu

7. Malalamiko yanayotolewa chinichini kutoka kwa wasimamizi wa zoezi la uhakiki, kuhusu posho zao na stahiki nyingine, ivyo kuongeza gharama za uendeshaji, overhead cost

8.Kuna dalili zote za kutokea kwa utaifishaji wa mali za wananchi kwa kisingizio cha kukomesha biashara ya kangomba.

Swali la kujiuliza kama wauzaji wa korosho hizo hawatalipwa na korosho zao zimechukuliwa na serikali, je hii tunaita nini?
Ni kweli kwamba hakuna wachuuzi wa mazao mengine zaidi ya korosho.

Hivyo ndugu waandishi, kutokana na masuala ya msingi niliyoyataja yanaweza kuwa na athari kubwa sana kwa mwananchi mmoja mmoja lakini athari kubwa iko kwa Taifa.

*Naomba niwatajie athari chache zinazoweza kujitokeza sasa hivi na baadae....*

1. Halmashauri zetu zitashindwa kujiendesha kwa sababu zinategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na mazao ikiwemo korosho, mtakumbuka kwamba mbaazi haikuwa na soko zuri msimu uliopita.

2. Kuharibika kwa korosho zilizoko maghalani kwa kunyeshewa na mvua, hasa zile zilizoko mikononi mwa wakulima, na hivyo kupoteza ubora wake ambao ndio sifa kuu ya korosho ya nchi yetu.

3. Wakulima kushindwa kujimudu maisha yao ya kawaida mfano kulipia ada za watoto (private schools) na michango mbalimbali hii pia itasababisha kushuka kwa elimu,  lakini pia wakulima hawa hawa wanashindwa kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu ujao, ivyo kupunguza uzalishaji, na baadae kipato kuendelea kushuka

4. Kupoteza mapato kwa serikali kwa maana ya *Export Levy na Export Revenue* hivyo kushusha thamani ya shillingi, na pia kupoteza imani kwa wafanya biashara wa nnje na wa ndani wa mazao.

5. Bidhaa kudorora madukani, hasa maduka ya vifaa vya ujenzi na vyakula kwasababu wafanyabiashara wakishajua ni wakati gani wakulima wanahitaji biadhaa fulani fulani.

7.Kujengeka kwa chuki  kati ya wananchi na serikali hasa kwa wale ambao watadhulumiwa korosho zao.

8. Kudorora kwa shughuli za maendeleo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambao kipindi kama hiki wananchi wanakuwa na kazi nyingi za maendeleo yao hasa ujenzi na uboreshaji wa makazi, na miundombinu mingine yakiwemo madarasa zahanati nk

Ni wakati sasa wa *Mh Rais* kutembelea mikoa ya Kusini na kuwapa wananchi nafasi ya kuzungumza ili ajionee mwenyewe ni kitu gani kinaendelea kwa lengo la kumsaidia mkulima na si vinginevyo
 
Imeandaliwa na;

*Cecil David Mwambe*(Mb)
*Mbunge Jimbo la Ndanda*
 
Mpekuzi.

Comments