Dk. Shein: Bahari kutumika kiuchumi .

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,  amesisitiza azma ya serikali ya kuanzisha taasisi ya utafiti ya uvuvi na mazao ya bahari, ili kwenda sambamba na sera ya uchumi wa bahari.
Hayo aliyasema jana wakati alipokutana na uongozi wa wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ikulu mjini Zanzibar ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alihudhuria ambapo uongozi huo ulieleza maendeleo ya miradi inayoendeshwa katika wizara hiyo.
Dk. Shein alieleza kuwa kuna umuhimu kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na taasisi ya utafiti ya uvuvi na mazao ya Bahari hasa ikizingatiwa mazingira ya Zanzibar na uchumi wake.
Alieleza kuwa ni jambo la busara kuwepo kwa taasisi hiyo ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa kwa Zanzibar na wananchi wake na kuipelekea Zanzibar kutekeleza ipasavyo uchumi wa bahari.
Alieleza kuwa tayari Zanzibar ni mwanachama wa Jumuiya ya nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IORA), hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati madhubuti katika kufikia malengo, makubaliano na maazimio ya Jumuiya hiyo ikiwa pamoja na kutekeleza kwa vitendo uchumi wa bahari.
Aidha, alieleza kuwa mbali ya uwepo wa Jumuiya hiyo ya (IORA) pia, Novemba mwaka jana 2018 alihudhuria mkutano wa uchumi wa Bahari uliofanyika mjini Nairobi kuanzia Novemba 26 hadi 28 ambapo mbali ya mambo mengine mkutano huo ulijikita na masuala ya uchumi wa bahari hasa kwa nchi zilizopakana na Bahari ya Hindi.
Alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha viwanda vya uvuvi hapa nchini, azma ya kuanzisha Chuo cha Ubaharia pamoja na kuiimarisha Kampuni yake ya  Uvuvi.
Akieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji, alisema kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kuongeza ukubwa wa eneo la kilimo cha umwagiliaji maji kwani mradi huo una umuhimu mkubwa kwa Wazanzibari hasa ikizingatiwa kuwa chakula cha wali ndio kilichopewa kipaumbele na jamii.

Comments