Dk. Shein atunuku nishani za mapinduzi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, ametunuku nishani ya Mapinduzi, nishani ya utumishi uliotukuka pamoja na nishani ya ushujaa kwa viongozi, watumishi wa umma, maofisa na wapiganaji wa idara za SMZ na wananchi wenye sifa maalum.

Hafla hiyo ilifanyika ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, serikali, wananchi pamoja na viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Awali akitoa tamko kuashiria kuanza shughuli hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Salum Maulid Salum, alisema Dk. Shein ametunuku nishani ya mapinduzi 45, nishani ya utumishi uliotukuka 53 na nishani ya ushujaa 14 kwa viongozi, watumishi wa umma, maofisa na wapiganaji wa idara za SMZ na wananchi.

Alieleza kuwa sherehe hiyo ilihudhuriwa na watunukiwa 112 ambao kati ya hao 40 ni marehemu ambao nishani zao zimepokelewa na wawakilishi wao na 72 wako hai ambapo nishani zao walipokea wenyewe au kupokelewa kwa niaba yao.

Alisema watunuku wote sifa zao zimekidhi matakwa ya nishani hizo ambapo nishani ya mapinduzi hutolewa kwa mtu ambaye aliasisi au alishiriki au aliyatukuza na kuyaenzi mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

Aliongeza kuwa mtunukiwa ni pamoja na kiongozi au mtu mwengine aliyehai au aliyefariki ambaye aliiletea sifa Zanzibar katika fani mbali mbali na kuonesha maadili mema ya kusifika na kuigwa ambapo katika sherehe hizo, nishani ya mapinduzi inatunukiwa katika kundi la viongozi na wananchi wenye sifa maalum.

Alisema nishani ya utumishi uliotukuka inatolewa kwa mtumishi wa umma au idara maalum za SMZ aliyehai au aliyefariki ambaye ametimiza utumishi wake kwa muda wa miaka isiyopungua 20 mfululizo na kwa mtumishi wa idara za SMZ miaka isiyopungua 20 ya kuwa ofisa na katika kipindi chote hicho amekuwa na tabia njema.

Aliongeza kuwa mtumishi huyo awe ametumikia taifa kwa uzalendo wa hali ya juu na kufanya kazi kwa kujitolea, uwajibikaji, uadilifu, ujasiri na umakini katika kusimamia majukumu na utendaji kazi.

Aidha, alieleza kuwa nishani ya ushujaa inatolewa kwa mtumishi wa idara maalum za SMZ au mtu mwengine yeyote aliyehai au aliyefariki ambaye ametenda kitendo cha ushujaa, ujasiri na uzalendo ambacho kimesaidia kuokoa mali au uhai wa mtu au kujitolea maisha yake kwa ajili ya ulinzi wa taifa.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa vitendo hivyo vya ushujaa viwe wazi ambavyo alivifanya na kuthibitishwa, mahala popote pale penye hatari na ameendelea kuwa muaminifu na mtiifu kwa nchi na serikali yake.

Nishani zilizotolewa ni pamoja na nishani ya mapinduzi kwa viongozi na wananchi wenye sifa mbali mbali akiwemo CP Ali Abdalla Ali, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Dk. Mohamed Seif Khatib, Said Bakari Jecha na Meja Mstaafu, Haji Abdalla Sadala.

Wengine ni Balozi Mohamed Mwinyi Mzale, Abdulrahman Mwinyi Jumbe, Masauni Yussuf Masauni, Abdalla Rashid Abdalla, Msham Abdalla Khamis, Biubwa Amour Zahor, Joha Shaali Khatib,  Sihaba Ismail Faraghani, Said Rashid Mohamed, Kombo Hassan Juma, Haji wa Haji wa Haji, Mohamed Iddi Juma, Amina Khamis Borafia.

Dk. Shein pia, aliwatunuku Khatib Idi Khatib, Mohamed Yahya Juma, Salum Hassan Mzee, Khamis Amour Mzee, Borafia Silima Juma, Kombo Ali Vuai, Salim Ali Matta, Juma Ali Juma, marehemu Rashid Mohamed Khamis, marehemu Haji Kombo Mbaraka, marehemu Othaman Bakari Othman na  marehemu Ame Mohamed Juma.

Wengine waliopewa nishani hizo ni marehemu Said Mwinyichande Mkanga, Safia Maneno Suleiman, marehemu Ali Khamis Suleiman (Ali Kima), marehemu Juma Othman Faki, marehemu Ramsa Mbarouk Foum, marehemu Hussein Ayoub Mussa, marehemu Hassan Faki Kombo na marehemu Jafari Ali Haji (Suwedi Mabugira), marehemu Omar Ussi Muhidini na marehemu Said Mussa Ali.

Aidha, Dk. Shein alitoa nishani ya Mapinduzi kwa timu za mpira na vikundi vya uhamasishaji vikiwemo timu ya Zanzibar Heroes 2017, timu ya Zanzibar ya mpira wa ufukweni 2017, bendi ya Safari Trippers na kikundi cha taarab cha Siti Binti Saad.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa nishani ya utumishi uliotukuka kwa watumishi wa serikali wakiwemo Balozi Hussein Said Khatib, Julius B. Raphael, Salmin Senga Salmin, Dk. Mohamed Saleh Jidawi, Uledi Mwita Kisumku, Khadija Ali Mohamed, Ahmed Himid Mbaye, Tamim Amour Hassan na Said Mohamed Hussein.

Comments