Alisema kitendo cha kuongeza vyanzo vipya ni kuongeza mzigo kwa
wananchi hivyo jambo la msingi ni kudhibiti mapato ya vyanzo vya sasa.
Akizungumza katika kikao cha kuibua mambo ya kuzingatia katika
utayarishaji wa bajeti kuu ya mwaka 2019,2020 kilichowashirikisha
watendaji wakuu wa serikali, serikali za mitaa na taasisi zinazohusiana
na ukuaji wa uchumi kilichofanyika hoteli ya Ngalawa, alisema lengo la
kikao hicho ni utekelezaji wa matakwa ya sheria namba 12 ya mwaka 2016
ambayo imetaka kuanzishwa kwa jukwaa la bajeti na uchumi.
Alifahamisha miongoni mwa maeneo yanayohitajika kupitiwa upya ni
pamoja na hali ya uchumi, mfumo wa mapato, vyanzo vya mapato
vinavyofanya kazi, matumizi ya fedha na changamoto zilizopo.
Pia alisema kutakuwa na utaratibu wa kuangalia sekta tatu
zilizogatuliwa ikiwemo elimu, afya na kilimo ili kuhakikisha kunakuwa na
urahisi wa upelekaji wa huduma za jamii na kufikia malengo ya serikali.
Alitaja eneo jengine ni uhaulishaji wa fedha kwa taasisi
zilizogatuiliwa ambapo unapaswa kufanywa kwa kuzingatia vigezo ikiwemo
idadi ya watu.
Sambamba na hilo, alisema eneo jengine litakaloangaliwa kwa umakini
ni pamoja na hali ya umasikini katika utafiti wa kaya uliofanywa mwaka
2014 -2015.
Kuhusu rasilimali watu wenye ujuzi, alisema kamati maalumu imeundwa
ya kuangalia eneo hilo na kupatiwa ufumbuzi sambamba na kamati ya
kuangalia sheria na mahitaji ya fedha kulingana na mahitaji.
Alisisitiza misingi ya uadilifu na uwajibikaji wenye kuzingatia
sheria za fedha na taratibu zilizopo katika vyanzo vya mapato ili kukuza
kiwango cha ukusanyaji.
Nae Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khamis Mussa Omar, alisema ugatuzi ni
miongoni mwa eneo muhimu la kufanyiwa tathmini ya haraka na kuangalia
changamoto zilizopo.
Alisema ugatuzi ni njia moja wapo ya kuharakisha upelekaji wa huduma za kijamii hivyo linahitaji kutekelezwa kwa weledi.
Nae Kamishna wa bajeti, Mwita Mgeni Mwita, alisema kikao hicho
kinapokea michango, maoni na mapendekezo yatakayokusanywa na kuingizwa
katika mkabala wa bajeti ambayo itapelekwa Baraza la Mapinduzi na Baraza
la Wawakilishi kwa ajili ya kujadiliwa na kuridhiwa.
Mchangiaji kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania, Saleh Haji,
alipendekeza kuandaliwa mfumo maalumu wenye kudhibiti mapato katika
maeneo ya bandari bububu.
Comments