Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limepinga kanuni mpya ya kukokotoa
mafao ya wastaafu iliyotolewa hivi karibuni likisema inakandamiza
wafanyakazi.
Shirikisho
hilo limesema pendekezo la wafanyakazi lilikuwa ni kuunganishwa kwa
mifuko ya hifadhi ya jamii na si kanuni mpya ya vikokotoo
inayolalamikiwa.
Mjadala
mkubwa unaendelea nchini baada ya kutangazwa kwa kanuni mpya za sheria
ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2014 ambazo zinaelekeza pamoja na
mambo mengine, kuwa wastaafu wote watalipwa mkupuo wa asilimia 25 ya
mafao pindi wanapostaafu na asilimia 75 inayobaki watakuwa wakilipwa
kama pensheni ya kila mwezi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mara baada ya kikao cha 35 cha shirikisho
hilo mjini hapa, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema kanuni hizo
ni kandamizi na zimepokewa na wafanyakazi kwa mtizamo hasi na zitashusha
ari yao na ufanisi.
“Kuunganishwa
kwa mifuko ni hoja ya Tucta tangu mwaka 2004 lakini kanuni mpya ni
kinyume cha mapendekezo yetu. Sisi tulitaka kanuni zibaki kuwa za mwaka
2017 ambapo kikokotoo ni 1/540 na mkupuo ni asilimia 50, huku wastani wa
umri wa kuishi ukiwa ni miaka 15.5,” alisema Nyamhokya.
Alisema
hoja ya ufanisi wa mifuko kwa mkupuo wa asilimia 50 hakutakuwa na shida
yoyote endapo Serikali italipa madeni yote ya mifuko na mifuko kuacha
uwekezaji usio na tija au kuuza kabisa.
Mamlaka
ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imewahi kufafanua
kuhusu deni hilo ikisema Serikali haijakopa katika mifuko ya hifadhi ya
jamii tangu mwaka 2013 kwa sababu tayari ilifikia ukomo ambao ni
asilimia 10 kwa mujibu wa mwongozo.
“Kwenye
vitabu vya Serikali madeni yake kwa mifuko ya hifadhi ya jamii bado
yapo. Serikali haijakana madeni yake tangu kuunganisha mifuko hii na
mara ya mwisho ilisema itatoa hati fungani ili kulipa hayo madeni yake,”
alisema Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka.
Mpekuzi.
Comments