Mamlaka
ya Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA) inaendelea kupokea maoni
mbalimbali kutoka kwa wadau na wananchi ambayo yatasaidia kuboresha
kanuni na miongozo itakayoendelea kumnufaisha zaidi mstaafu kupitia
mafao yake.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es salaam jana,
Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Dk. Irene Isaka, alisema lengo la mamlaka hiyo
ni kuendelea na maboresho ya kanuni na miongozo, kwani dirisha la maoni
lipo wazi kwa watanzania kuleta mawazo yao yatakayosaidia
kuboresha mfumo wa mafao kwa wastaafu.
“Milango
ipo wazi kwa wananchi na wadau mbalimbali kuleta maoni yao, ili
tuboreshe sheria na kanuni zinazoongoza mifuko ya jamii na kuongeza tija
katika mafao ya wastaafu,’’ alisema Dk. Isaka.
Alieleza
kuwa kanuni zinazotumika sasa zimetokana na ushirikishwaji wa wadau
mbalimbali wakiwemo wafanyakazi, waajiri na kwa ujumla katika kutoa
maoni na mapendekezo yamesaidia kupatikana kwa sheria na kanuni ambazo
zimeleta neema kwa wastaafu kwa kupata mafao stahiki na kwa wakati.
“Taratibu za mafao zinampa mstaafu nafasi ya kupata mkopo
katika
baadhi ya benki nchini kutokana na uhakika wa pensheni yake kwa kipindi
cha kustaafu kwake na kumfanya aweze kuendelea kufanya miradi
mbalimbali ya maendeleo,” alisema.
Dk.Isaka
alisema tofauti na miaka ya nyuma pensheni za wastaafu zilikuwa na
ukomo wa muda wa miaka 10 mpaka miaka 12, lakini kwa kanuni za sasa
pensheni ya mstaafu atapokea kwa kipindi chote cha maisha yake ya
kustaafu, hii inampa uhakika wa kupata mkopo na kuendelea kufanya
shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Moja
ya majukumu ya SSRA ni kulinda na kutetea maslahi ya mwanachama wa
mifuko ya hifadhi ya jamii hivyo tutaendelea kupokea maoni ili
mwanachama anufaike zaidi kupitia michango yake atakapostaafu,” alisema.
Alisema
SSRA itaendelea kuwaelimisha wanachama na wananchi kwa ujumla juu ya
kanuni mpya ya ukokotoaji na faida zake kwa wanachama pale atakapo
staafu, kwani imeonekana uelewa wa hii kanuni mpya haijawafikia watu
wengi nchini na hata wale wachache waliofikiwa na taarifa hiyo wengi wao
wamepotoshwa.
“SSRA tumejipanga kuwafikia wanachama wote nchini na
kuwapa
elimu juu ya kanuni hii mpya ya ukokotoaji wa mafao ili kuwaondoa
katika hofu ambayo imejengeka miongoni mwao kutokana na maneno ya baadhi
ya watu wasio na uelewa wa kutosha juu ya kanuni mpya ya Ukokotoaji
mafao,” alisema Dkt. Isaka.
Alisema
madhumuni ya mamlaka hiyo ni kumuondoa mstaafu katika hali mbaya ya
kiuchumi baada ya kumaliza mafao yake ya mkupuo ya asilimia 25, kwa
kumpatia asilimia zilizobaki kama pensheni ya kila mwezi kwa kipindi
chote cha maisha yake.
Mpekuzi.
Comments