Mkataba mgawanyo mafuta umefuata sheria-AG.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema suala la utiaji saini mkataba wa mgawanyo wa mafuta (PSA) haukufanywa kisiasa bali ulifanywa kisheria.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Said, alieleza hayo ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, wakati akitoa ufafanuzi kwa hoja iliyowasilishwa na Mwakilishi wa jimbo la Kikwajuni, Nassor Salim Ali (Jazira) juu ya kuunga mkono hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuingia katika mkataba wa ugawaji wa mafuta.

Alisema utiaji saini mkataba huo ulifanywa kwa sheria na kufuata kanuni, hivyo ni vyema wananchi kujua umuhimu wa mkataba huo.

Alisema wapo wananchi ambao wameanza kubeza mkataba huo baada ya kupata taarifa kuwa mafuta yatakayopatikana yatakuwa ya mgao na Zanzibar haitanufaika kwa asilimia kubwa.

Alisema wananchi wa Zanzibar watapata asilimia 70 ya mgao unaotokana na raslimali hiyo na sio kugawiwa sawa sawa kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi.

Aidha aliwaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wananchi kuacha kusikiliza propaganda za kupotosha juu ya mkataba huo.

Aliwahimiza wawakilishi kuzisoma sheria na kuacha kusikiliza maneno ya mitaani ya upotoshaji ambayo yana nia mbaya.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, akifafanua juu ya hoja hiyo alisema wapo watu wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanakwamisha utafiti wa mafuta na gesi lakini wameshindwa.

Alisema mapato ambayo yatapatikana katika sekta hiyo yatawasaidia wananchi ambapo wazanzibari wameanza kunufaika tangu kutiwa saini mkataba huo.

Mapema wakichangia hoja hiyo, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, walimuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kutia saini mkataba wa mgawanyo wa uzalishaji wa mafuta.

Walisema Dk. Shein anastahili kupongeza kutokana na kujali maslahi ya wananchi anaowaongoza.

Zanzibarleo.

Comments