Lugola Awataka Polisi Kuimarisha Ulinzi Msimu Wa Sikukuu.....Aagiza Vibaka, Matapeli Na Majambazi Wakamatwe.
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelitaka Jeshi la Polisi
nchini liimarishe ulinzi wakati wa sikukuu za krismasi na mwaka mpya na
kuwataka wananchi kutokujisahau kwasababu ya sikukuu hizo.
Akizungumza
na Wananchi wa Kijiji cha Kisorya, Kata ya Kisorya, Jimbo la Mwibara,
Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo,
alisema msimu huu wa sikukuu vibaka, majambazi na matapeli hutumia
sikukuu hizo kufanya uhalifu.
Alisema
Polisi wanapaswa kujipanga zaidi ili kuhakikisha sikukuu hizo
zinasherekewa kwa amani kwa kufanya ulinzi kona zote za nchi ili
wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa usalama na kuendelea kuijenga
nchi yao.
“Hili
tatizo la kuwepo vibaka na kuwafanya wananchi waishi kwa wasiwasi
nchini, sasa napenda niwaambie nyie wananchi wa hapa Kisorya, na
Tanzania kwa ujumla, Jeshi lipo imara, hao vibaka pamoja na majambazi
wote, sasa hawana nafasi, nawaagiza polisi kufanya msako mkali
kuwakamata matapeli, vibaka na majambazi wanaojitokeza hasa kipindi hiki
cha maandalizi za sikukuu za krismasi na mwaka mpya, “ alisema Lugola.
Pia
Lugola aliwataka wananchi watoe taarifa polisi iwapo wataona dalili
zinazoashiria uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ili Jeshi la
Polisi liweze kuzifanyia kazi mapema taarifa hizo.
Aidha,
Lugola aliwataka Polisi nchini kuwakamata watu wanaowarubuni wanafunzi
pamoja na kuwatia mimba, wawafungulie mashtaka haraka iwezekanavyo
kutokana na tatizo hilo kushika kasi nchini na kuwafanya wanafunzi
kukatisha masomo yao.
“Wananchi
wa Kisorya, tatizo hili ni la nchi nzima, na mara kwa mara nalikemea na
kuwapa maagizo polisi kuwakamata watu wanaoharibu watoto wadogo wa
shule kwa kuwatia mimba, nawataka polisi muwe wakali sana kuhusu hilo,
hakuna kucheka na mtuhumiwa, kamateni wekeni rupango na apelekwe
mahakamani mtuhumiwa ili kukomesha tatizo hili sugu hapa nchini,”
alisema Lugola.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, alikiri tatizo
hilo kuwa sugu wilayani humo, hata hivyo alimuahidi Waziri Lugola
watalishughulikia na wahalifu wote watakamatwa.
“Mheshimiwa
Waziri, matatizo ya wananfunzi kutiwa mimba hili lipo wilayani hapa,
ila siku za nyuma tuliwahi kumkamata mwalimu ambaye alimtia mimba
mwanafunzi na baadaye akasingizia kuwa mimba hiyo siyo yake na alipigwa
na mwanafunzi mwenzake, hivyo tupo wakali kuhakikisha tunalimaliza
tatizo hilo kwa kuwakamata na kuwapeleka mahakamani watuhumiwa,” alisema
Bupilipili.
Pia
katika mkutano huo, Waziri Lugola aliwataka wananchi wa jimbo lake
waanze maandalizi ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuepuka
janga la njaa lisije likawakumba endapo hawatalima. Hata hivyo, kijiji
hicho alichokitembelea, kwa mujibu wa taarifa ya mipango yao ya kilimo
walisema kuwa wana upungufu mkubwa wa mbegu za mazao mbalimbali hasa zao
la pamba.
“Nimeagiza
maafisa ugani waje kuangalia upungufu wa mbegu za pamba na kutatua kero
hii kutokana na taarifa yenu ya mpango wa kilimo ya mwaka 2018/2019, na
pia nasisitiza zaidi mlime mazao ya chakula kwa wingi,” alisema Lugola.
Lugola
anaendelea na ziara jimboni kwake akisikiliza kero za wananchi pamoja
na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi, mpunga, viazi na
mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao hayo kwa wingi.
Mpekuzi.
Comments