Duru ya kwanza ya mazungumzo ya Sahara Magharibi yafanyika kwa mafanikio.

Duru ya kwanza ya mazungumzo ya Sahara Magharibi yafanyika kwa mafanikio Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Morocco na harakati ya Polisario kuhusu mzozo wa eneo la Sahara Magharibi yaliyozishirikisha Algeria na Mauritania imemalizika kwa wajumbe wa mazungumzo hayo kuridhishwa na mchakato huo.

Mazungumzo hayo kati ya Morocco na harakati ya Polisario kuhusu mzozo wa Sahara Magharibi yalifanyika jana katika kikao cha faragha kwa kuhudhuriwa na Horst Koehler, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya eneo la Sahara Magharibi. 

Ripoti zinaonyesha kuwa, mazungumzo ya awali kuhusu mzozo wa Sahara Magharibi yamekuwa na matokeo ya kuridhisha.  

Koehler amesema anataraji kuwa mazungumzo hayo ambayo yalikwamza tangu mwaka 2012 yatahuishwa upya na itapatikana njia ya ufumbizi itakayoridhiwa na pande zote mbili husika ili kuhitimisha mzozo wa Sahara Magharibi.

Harakati ya Polisario imekuwa ikiiendesha mapambano tangu mwaka 1973 ya kupigania uhuru  wa eneo la Sahara Magharibi kutoka kwa Morocco. 

Mapigano kati ya serikali ya Morocco na harakati ya Polisario yalianza mwaka 1975 na mwaka 1993 kulitiwa saini makubaliano ya kusitisha vita kati ya pande mbili hizo chini ya usimamizi wa  Umoja wa Mataifa.
 
Serikali ya Morocco inataka kuibakisha Sahara Magharibi chini ya mamlaka yake na kuipatia mamlaka ya utawala wa ndani. Hata hivyo harakati Polisario inapinga mpango huo na inatoa wito wa kuitishwe kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo hilo.  

parstoday.

Comments