Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini (DPP), bado anasubiri mwenendo wa uamuzi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, uliotupilia mbali pingamizi lake la awali
dhidi ya rufani ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko,
wanaoendelea kusota mahabusu.
Novemba
30, mwaka huu Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam,
ilisikiliza pingamizi la awali la DPP la kutaka rufani ya kupinga
kutenguliwa dhamana ya walalamikaji Mbowe na Matiko isisikilizwe,
itupiliwe mbali.
Hata
hivyo, walalamikaji kupitia mawakili wao, Peter Kibatala, Jeremia
Mtobesya na Dk. Rugemeleza Nshala, waliiomba mahakama kutupilia mbali
pingamizi hilo.
Mahakama
hiyo iliyoketi chini ya Jaji Sam Rumanyika, ilikubaliana na hoja za
walalamikaji kwa kutupilia mbali pingamizi la mlalamikiwa DPP, kwamba
halina mashiko kisheria.
Mlalamikiwa hakuridhika na uamuzi huo aliwasilisha kusudio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Jaji Rumanyika.
Jaji Rumanyika alisitisha mwenendo wa kesi hiyo hadi Mahakama ya Rufani itakaposikiliza na kutoa uamuzi wa rufani ya DPP.
Mbowe
na Matiko wamekata rufani Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Hakimu Mkazi
Mkuu, Wilbard Mashauri wa kuwafutia dhamana kwa sababu waliidharau na
kukiuka masharti ya dhamana ya mahakama hiyo.
Walifutiwa
dhamana kwa madai kwamba hawakufika mahakamani kuhudhuria kesi
inayowakabili ya uchochezi, Novemba Mosi na 8, mwaka huu na taarifa za
kutokuwapo zilikinzana.
Mbowe na Matiko walipelekwa mahabusu na kesi ya msingi itatajwa Desemba 6, mwaka huu.
Mpekuzi.
Comments