Wanafunzi 16,709 kidato cha nne kutahiniwa Zanzibar.

JUMLA ya vituo 212 vinatarajiwa kufanyiwa mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne katika skuli za Zanzibar ambapo watahiniwa 16,709 wanatarajiwa kufanya mitihani kuanzia Novemba 5 hadi Novemba 23 mwaka huu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, aliyasema hayo, alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, juu masuala ya ufanyaji wa mitihani kitaifa.
Alisema kati ya vituo hivyo, skuli za serikali zitakuwa na vituo 164 ambapo 94 vinatarajiwa kuwepo Unguja na 70 vitakuwa Pemba huku kwa skuli binafsi kutakuwa na vituo 48 ambapo 42 Unguja na Vituo 6 vitakuwa kwa skuli za Pemba.
Alisema kati ya wanafunzi hao, skuli za serikali jumla ya wanafunzi wanatarajiwa kuwa ni 14,709 wakiwemo wanawake, 8,569 na wanaume 6,210 huku skuli binafsi wanatarajiwa kuwa 1,930, wanawake ni 1,060, na wanaume 870.
Aidha waziri huyo, alisema katika kipindi chote cha mitihani hakutaahirishwa mtihani wowote kwa kisingizio cha uwepo wa mvua, hivyo aliwatawa wazazi, walezi na wananchi kuwa karibu na watoto wao kipindi chote cha ufanyaji wa mitihani sambamba na kuchukua jukumu la kumuwahisha mwanafunzi katika kituo cha mitihani ili aweze kupata nafasi ya kufanya mitihani yake kama ratiba ilivyopangwa.
Akizungumzia upande wa wanafunzi wa kidato cha pili, alisema kuwa mitihani hiyo inatarajiwa kufanyika mara baada ya kumalizika kwa mitihani ya kidato cha nne ambapo kwa mitihani ya kidato cha pili inatarajiwa kuanza Disema 3 hadi Disema 11 mwaka huu.
Aidha alisema kuwa darasa la nne mitihani yao inatarajiwa kuanza Novemba 21, kwa upande wa darasa la sita mitihani yao inatarajiwa kufanyika Novemba 26 mwaka huu.
Zanzibarleo.

Comments