Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, amesema serikali ipo
katika hatua nzuri ya kukamilisha hatua za ujenzi wa bandari ya uvuvi na
kununua meli kwa ajili ya kuvua samaki kwenye eneo la bahari kuu pamoja
na kuziwezesha meli nyingine kutia nanga katika bandari hiyo ikiwa ni
lengo la Tanzania kwenda sambamba na nchi nyingine duniani kukuza uchumi
kupitia sekta ya uvuvi.
Mhe.
Ulega amebainisha hayo mara baada ya kuwasili nchini akitokea Mjini
Nairobi nchini Kenya, ambapo hivi karibuni amehudhuria mkutano
uliowajumuisha wajumbe zaidi ya elfu nne, kutoka mataifa mbalimbali,
ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli
amewakilishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindudi
Dkt. Ali Mohamed Shein.
Mhe.
Ulega amesema mchango wa sekta ya uvuvi hapa nchini bado ni mdogo hivyo
mkutano huo umeongeza hamasa kwa Tanzania kutafuta namna bora ya ukuaji
uchumi kupitia sekta ya uvuvi.
“Sisi
tuko katika hatua nzuri ya kuweza kukamilisha ujenzi wa bandari ya
uvuvi, tukishafanikiwa kujenga bandari ya uvuvi, maana yake ni kwamba
meli zitatia nanga hapa kwetu, tutapata ajira, tutatengeneza pia vile
vile maeneo ya kuhifadhia samaki kwa wingi, tutachakata, tutakuwa na
uwezo wa kuuza katika soko la ndani na soko la nje.” Alisema Mhe. Ulega
Aidha,
amesema serikali imeshaanza hatua ya ununuzi wa meli zake zenyewe,
hatua iliyoilazimu kulifufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) ambalo tayari
limeshaanza kufanya kazi.
“Ili
uchumi wenyewe uwe endelevu ni lazima kulinda mazingira ya bahari,
maziwa, mito, kulinda rasilimali zilizopo humo, ndio maana Tanzania
inafanya kazi ya ulinzi wa rasilimali hizo ili ziwe endelevu hata kwa
vizazi vijavyo viweze kukuta na kuzuia uchafuzi wa mazingira hayo pamoja
na uvuvi usiofuata sheria.” Alisema Mhe. Ulega
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema pia katika
mkutano huo wa ‘Blue Economy’ wenye lengo la kukuza uchumi kupitia sekta
ya uvuvi uliofanyika Mjini Nairobi nchini Kenya, umebainisha kuwa sekta
ya utalii ni muhimu katika uchumi endelevu, sambamba na ulinzi na
usalama wa nchi, pia kuzuia uingizwaji wa dawa za kulevya ambazo
zimekuwa zikiingizwa katika mataifa mbalimbali kupitia njia ya bahari.
Mwisho.
Imetolewa na: Edward Kondela
Afisa Habari-Wizara ya Mifugo na Uvuvi
28.11.2018.
Mpekuzi.
Comments