MWENYEKITI
wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Mbunge wa Vunjo, James Mbatia
amewamegea siri wananchi wa mji mdogo wa Himo juu ya mazungumzo yake na
Rais Dk. John Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Alidai
alikwenda kumueleza malalamiko ya wananchi kuhusu amri ya Mkuu wa
Wilaya ya Moshi ya kusitisha ujenzi wa barabara na kusababisha hasara ya
mabilioni ya shilingi.
“Haya
yote nimemueleza Mheshimiwa Rais (Magufuli) niwe mkweli, nilibahatika
hapo katikati Mheshimiwa Rais akaniita akasema hivi, narejea sauti ya
Rais aliniambia na ameshaagiza ofisi zake na wengine wameniita Dodoma,
barabara za wana Vunjo atachangia yeye binafsi kama John Pombe Magufuli,
pili serikali yake itachangia na tatu atakuja kama Amiri Jeshi Mkuu
kufungua barabara hizi yeye mwenyewe kama John Pombe Magufuli,”alisema
Mbatia
alikuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Makuyuni katika Mamlaka ya
Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi wakati wa mkutano wa hadhara
uliofanyika viwanja vya ghalani.
Mradi
wa upanuzi na ujenzi barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe
unaodaiwa kusisitishwa katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro,
unahusisha barabara zenye urefu wa kilometa 389.3 ambazo zilikuwa
zigharimu Sh. bilioni 12.077 kutokana na utafiti wa Wakala wa Barabara
za Vijijini na Mijini (Tarura) wa mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba anadaiwa kusimamisha kazi ya ujenzi wa barabara hizo na hivyo kusababisha hasara.
Zaidi
Mbatia alisisitiza: “Sasa tuone ni nani zaidi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na maendeleo ya watanzania, maendeleo hayana
itikadi za vyama. Kwa nini amefanya hivyo, kwa sababu Jimbo la Vunjo
tumekuwa wa kwanza Tanzania kuweza kujipanga wenyewe mpaka hatua
tuliyofikia ya kujiletea maendeleo yetu wenyewe na tujipongeze wana
Vunjo.
"Hizi
barabara zikiwa vizuri si tunazitumia sote, barabara za Makuyuni zikiwa
nzuri zitaendelea kutumiwa na watu wote hata kama Mbatia sitakuwa
Mbunge…Mimi sijawahi kumtukana Rais, sasa atakuja yeye mwenyewe.”
Mbatia
alikutana na Rais Magufuli na kufanya mazungumzo naye Ikulu, Novemba 13
mwaka huu akiwa pamoja na wanasiasa wengine Mh. John Cheyo (UDP), John
Shubuda na mfanyabiashara Rostam Aziz.
Katika
mkutano huo, Mbatia aliwaeleza wananchi hao kwamba amekopa fedha zaidi
ya Sh. milioni 500 Benki ya CRDB kwa ajili ya kununua mitambo ya ujenzi
wa barabara hizo.
“Mimi
nimenunua mitambo sawa, mingine tunakodisha sawa lakini tukasema
wananchi waanze kuchangia mafuta kwenye hiyo mitambo hiyo, kwa mfano
Kijiji cha Mshihiri mpaka leo hii wameshachangia takribani Sh. milioni
26 lakini ukichanganya zote pamoja na za Ashira ni zaidi ya Sh. milioni
30 na kitu huko,”alieleza
Akijibu
maswali ya wananchi kuhusu kukwama kwa ujenzi wa barabara za
Samanga/Sembeti, Mbunge huyo alisema Mungu sio Athuman na akawataka
wananchi hao kusubiri kwanza ili mdomo wake usiteleze kwa vile wana kesi
mahakamani.
Wakati
anahitimisha mkutano huo, Mbatia aliipongeza Kamati ya Maendeleo ya
wana Vunjo (VDF) chini ya Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini
Dk. Martin Shao, mashekhe wetu, mapadri wetu na wachungaji na viongozi
wote, akisema yeye binafsi toka sakafu ya moyo wake hana chuki na mtu
yeyote na anamshukuru Mungu amesikia na Mheshimiwa Rais (Magufuli)
amesikia dua zao.
Mpekuzi.
Comments