Hatua za upande mmoja za Marekani, tishio kwa misingi ya ushirikiano wa kimataifa na wa pande kadhaa.

Hatua za upande mmoja za Marekani, tishio kwa misingi ya ushirikiano wa kimataifa na wa pande kadhaaAwamu ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran iliyoanza kutekelezwa Novemba 5 wiki iliyopita imekabiliwa na upinzani wa walimwengu.

Upinzani huo unatokana na kuwa, siasa hizo za upande mmoja na za ukiukaji wa mapatano za Marekani zinakinzana moja kwa moja na utawala wa sheria pamoja na misingi ya hati ya Umoja wa Mataifa na ya pande kadhaa. 
Kimsingi ni kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa, Marekani ambayo ni nchi mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama yenye haki ya kura ya veto, inayaadhibu mataifa mengine si kwa sababu ya kukiuka moja ya maazimio ya Baraza la Usalama, bali kwa sababu ya kuheshimu na kuyakeleza maazimio hayo.
Mwenendo na hatua hizi za upande mmoja, za kijuba na zenye jeuri ndani yake za Marekani ambazo zimejikita katika 'dunia iliyojengeka juu ya misingi ya nguvu badala ya utawala wa sheria' ni tishio kwa ulimwengu. 
Gholamali Khoshroo, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa akihutubia hivi karibuni katika Baraza la Usalama alikosoa vikali siasa za upande mmoja za Marekani na kusema: Siasa za jeuri na kujiona sambamba na hatua za upande mmoja za Marekani zimekuwa zikihatarisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa na wa pande kadhaa.
Swali lililopo kwa sasa ni hili kwamba, je, jamii ya kimataifa imeweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika kukabiliana na hatua za upande mmoja za serikali ya Washington? Kuhusiana na jambo hilo, filihali macho na masikio ya walimwengu yameelekezwa kwa Umoja wa Ulaya ambao ni moja ya pande husika katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Maja Kocijancic, msemaji wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya kigeni anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba:
Juhudi za kuyalinda makubaliano ya nyuklia na Iran na kadhalika kuhifadhi mahusiano ya kibiashara na kiuchumi na Tehran hususan hatua ya kuanzisha mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha na Iran, zimeonekana kuchukua kasi katika majuma ya hivi karibuni.
Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo, mfumo wa SWIFT wa mawasiliano ya kibenki umetangaza kwamba, mawasiliano ya baadhi ya benki za Iran na mfumo huo yatakatwa. 
Hii ni katika hali ambayo, nukta za kina za kuanzishwa kanali maalumu ya kifedha ambayo imeahidiwa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuyawezesha mashirika ya Ulaya kukwepa vikwazo vya Marekani na kusaidia kuendelea kufanya biashara na Iran bado hazieleweki.
Sayyid Kamal Kharrazi, Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema kuwa: Mikakati ya pande kadhaa ya Umoja wa Ulaya ambayo imo katika hali ya kufanyiwa kazi, ina mwendo wa kinyonga na endapo hilo halitafanikiwa, kutaibuka matatizo na madhara makubwa. Katika hatua ya awali maeneo ya Mashariki ya Kati na Ulaya ndiyo yatakayopata hasara na kisha ulimwengu kwa ujumla.
Kwa hakika kile ambacho kiko wazi ni kuwa, kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kisha kurejeshwa vikwazo vya upande mmoja vya Washington dhidi ya Tehran kunakinzana wazi na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aidha hatua hiyo inakwenda kinyume kabisa na sheria za kimataifa.
Akizungumza hivi karibuni, mwishoni mwa kikao cha pamoja cha wakuu wa Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola mjini Tehran, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: Shabaha kuu ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo visivyo halali na kuulenga mfumo wa benki, usafirishaji mafuta na baadhi ya bidhaa za taifa hili zinazosafirishwa nje ya nchi, ni kutaka kuacha athari mbaya na hasi katika maisha ya wananchi wa Iran.
Hata hivyo, wananchi wa Iran wameishinda mipango na njama za Marekani kwa kusimama kwao kidete. 
Wamarekani walikuwa wakidhani kuwa, tarehe 5 Novemba iliyokuwa siku ya kuanza duru mpya ya vikwazo dhidi ya Iran ungekuwa mwanzo wa kutimia ndoto na matumaini yao lakini wananchi wa Iran wamesambaratisha ndoto yao hiyo. 
parstoday.

Comments