Tanzania ina upungufu madaktari wa macho.

TANZANIA ina madaktari bingwa wa macho 55 ambao wanatoa huduma kwa watu zaidi ya milioni 50.
Hiyo ni sawa na wastani wa daktari mmoja kwa watu milioni moja, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na wastani wa dunia unaotaka daktari mmoja kuhudumia watu 400,000.
Kaimu Rais wa Madaktari wa Macho nchini, Dk. Cyprian Gabriel alisema idadi ya madaktari hao pia ni wale walioko mijini lakini wanakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba wakati vijijini hawana kabisa huduma hizo.
Alitoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa ya ugonjwa wa macho  jana  jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya macho duniani. “Mheshimiwa mgeni rasmi, tatizo ni kubwa kuliko watu wanavyofikiria, madaktari ni wachache wakati tatizo ni kubwa zaidi vijijini,” alisema.
Aidha alisema tatizo la watu wengi kujiita ni madaktari bingwa wa macho wakati ni vishoka na wamekuwa wakisababisha usugu wa maradhi kwani wanapotibu watu huwa wanawaumiza zaidi.
Kaimu mganga mkuu wa serikali, Dk. Eliud Eliakimu, alisema tatizo la macho ni kubwa duniani kote kwani takwimu zinaonyesha watu 255 milioni wanaugua macho duniani.
Aliomba vishoka wanaotibu macho kusakwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwani wanakuwa chanzo cha upofu kwa watu hata pale ambapo wangeweza kutibika.
Zanzibarleo.

Comments