Serikali yasisitiza uchumi wa viwanda kuimarisha kipato cha wananchi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,Serikali imechagua kujenga uchumi wa viwanda utakaoifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Mipango na miradi mbalimbali imeanzishwa na inatekelezwa na Serikali kutimiza lengo hilo. Baadhi ya miradi hiyo ni wa kufua umeme wa Stigler’s Gorge utakaozalisha megawati 2,100 na mradi wa reli ya kisasa (SGR) utakaosafirisha abiria na mizigo mingi zaidi.
Serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia wawekezaji nwa ndani na nje. Imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuanzisha kituo cha pamoja cha huduma kilichopo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Jukwaa la Fikra linaloandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) lililofanyika Oktoba 4 na kuwakutanisha wadau waliojadili fursa, changamoto na matokeo ya kuwa na uchumi wa viwanda ni miongoni mwa mikakati ya kufanikisha sera hiyo.
Msingi mkuu wa majadiliano hayo ulikuwa kupendekeza suluhisho kwa vikwazo vinavyokwamisha harakati za ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuona matokeo chanya ya uchumi huo kwa Watanzania.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage anasema miaka ya nyuma Serikali ilitaka kufanya kila kitu bila kushirikisha sekta binafsi na inatambua ilifanya makosa ndiyo maana sasa inaishirikisha sekta binafsi.
Mwijage anasema Serikali inalenga kujenga uchumi wa kitaifa ili wananchi wawe na maisha mazuri ifikapo mwaka 2025 na maisha hayo yanatafsiriwa kwa kuwa na wastani wa pato la Dola 3,000 za Marekani kutoka wastani wa Dola 1,000 sasa hivi kwa mwaka.
Mbali na kuwa na uchumi jumuishi, Mwijage anasema hadi mwaka 2025, Tanzania inatakiwa kuwa Taifa ambalo watu wake wana elimu, lenye uchumi shindani na utawala bora.
Anasema mpango wa maendeleo wa miaka mitano unalenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu yanayopimwa kwa elimu, kipato na afya.
“Ili uweze kujenga huu uchumi, tumejielekeza kwenye viwanda. Tunataka kujenga uchumi jumuishi wa viwanda,” anasema Mwijage.
Waziri huyo anasema Serikali imeamua kujenga viwanda vilivyo katika makundi matatu; kwanza ni vinavyotumia malighafi zinazozalishwa na Watanzania wengi. Anasema hiyo ndiyo dhana ya kujenga uchumi jumuishi kwa kuwa kila mwananchi ataguswa na uchumi huo.
Pili, anasema ni viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa wingi. Mwijage anasema viwanda hivyo vitasaidia kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo zinatumika kuagiza bidhaa nje ya nchi na kuongeza uwezo wa kuuza nje ya nchi.
“Tunataka kujenga uwezo wa kuuza bidhaa nje ya nchi. Kwa sasa tunajitegemea kwenye saruji, tunazalisha tani milioni 10.8 wakati mahitaji ya ndani ni tani milioni 4.8, hiyo ziada tunauza nje ya nchi. Tunataka iwe hivyo kwenye maeneo mengine pia,” anasema waziri huyo.
Tatu, Mwijage anasema viwanda vingine ni ambavyo vinazalisha ajira kwa wingi, mfano sekta ya pamba na sukari. Anatolea mfano Kiwanda cha Sukari cha Kagera ambacho kina uwezo wa kuzalisha tani 75,000 kwa mwaka na kuajiri wafanyakazi 6,000.
Waziri huyo, mbunge wa Muleba Kaskazini anasema Tanzania inaweza kuzalisha tani milioni mbili za sukari na kutosheleza mahitaji yake ya ndani na ziada kuuzwa nje ya nchi kama ilivyo kwenye saruji.
Anasisitiza sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda vidogo ili kuimarisha uchumi wa viwanda na kufanya sekta ya viwanda kuwa mhimili wa uchumi wa Taifa. Anasema awamu ya kwanza ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano ilikuwa ni kuondoa vikwazo vya uwekezaji lakini sasa wanajenga viwanda.
Mkurugenzi wa maendeleo na biashara wa kampuni ya General Electric International, Gilman Kasiga anasema viwanda vikubwa vitachochea ukuaji wa viwanda vidogo nchini na kuunganisha uchumi huo na biashara nyingine.
Anasema uchumi wa viwanda utasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania hasa katika kipindi hiki ambacho vijana wengi wanamaliza elimu ya juu lakini wanakosa ajira. Anasema wakiunganishwa na uchumi wa viwanda watapata fursa mbalimbali za ajira.
Mkurugenzi huyo anabainisha kwamba uchumi wa viwanda pia utasaidia kukuza Pato la Taifa (GDP) na kuiwezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya, maji na kujenga miundombinu muhimu.
“Nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo, zilifika hapo baada ya kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda. Hatuwezi kuendelea bila kuwa na uchumi imara wa viwanda,” anasema Kasiga ambaye ameshiriki kuandika kitabu kinachohusu uchumi wa viwanda Tanzania pamoja na Ali Mufuruki.
Mkurugenzi wa kampuni ya KPMG, Alexander Njombe anasema ni muhimu wananchi wawe tayari kushiriki uchumi wa viwanda ili kubadili uchumi wao.
Njombe anasema ukosefu wa mtaji kwa wananchi ni kikwazo kwao kunufaika na maudhui ya kijamii (local content).
“Serikali iliongeza sekta kwenye sheria ya local content, sekta hizo ni viwanda na biashara, kilimo, mifugo na uvuvi, usafirishaji na mawasiliano na nishati. Kitu muhimu sasa ni jinsi ya kutekeleza yaliyomo kwenye sheria hiyo,” anasema Njombe.
Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye anasema changamoto kubwa katika ubia kati ya Serikali na sekta binafsi ni kutoaminiana, jambo linalodhoofisha ushirikiano baina yao.
Simbeye anasema Tanzania imekuwa na ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) na sheria zimekuwa zikibadilishwa kila mara lakini hakuna miradi ya ubia inayotekelezwa.
Anasema matamshi ya baadhi ya viongozi yanawaona wawekezaji kama watu wasio waaminifu na wanaolenga kupora rasilimali za nchi, jambo ambalo si kweli.
“Tatizo kubwa linalokwamisha miradi ya ubia ni upatikanaji wa mtaji hasa wa muda mrefu. Waziri umekuwa ukifanya kazi ya kutatua changamoto mbalimbali, tunaomba utumie muda wako kubuni vitu vingine vipya,” anasema Simbeye.

Comments