Kajubi awapa mbinu wanahabari.

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, amesema upo umuhimu kwa vyombo vya habari kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki yenye kufuata maadili ya utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Alisema hayo wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa  kujadili kusinyaa kwa  nafasi za asasi za kiraia na vyombo vya  habari uliofanyika hoteli ya Ocean View Kilimani.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuondosha tatizo la kusinyaa kwa uhuru wa vyombo vya habari ambalo kwa sasa limekuwa  likijitokeza dunia nzima.

Aidha alisema vyombo vya habari vina umuhimu na nafasi kubwa kwa taifa kutokana na mchango wao hususan katika kusukuma masuala ya maendeleo na jambo la msingi ni ushirikiano kwenye maeneo ya kazi  ili kuleta tija ya  uwajibikaji.

Nae Kiondo Reubet Mshana, alisema waandishi wa habari wanapaswa kujilaumu wenyewe kutokana na mwenendo wao ambao mara kadhaa umekuwa ukikiuka maadili na taratibu zao za kazi.

Kuhusu kufungwa kwa baadhi ya vyombo vya habari, alisema unatokana na ukosefu wa taarifa sahihi ambazo zimekosa uchunguzi na vielelezo vyenye ushahidi wakati wanapoandika habari.

Alisema, mwandishi wa habari lazima ajikubalishe kujituma kwa weledi,ufasaha kwa kufuata maadili ya kazi yake na sio kujenga tabia ya kuilaumu serikali kwa mambo yasio na msingi.

Mwanasheria Hardlod Sungusia, alisema katiba za Zanzibar na Tanzania zimeeleza umuhimu wa wananchi kupata habari huku maadili na taaribu kwa vyombo vya habari zikihimiza umuhimu wa uhuru, haki na kuzingatia utawala wa sheria.

Zanzibarleo.

Comments