Jeshi la Polisi lamwekea ulinzi Mo Dewji.

Jeshi la Polisi limemwekea ulinzi mfanyabiashara maarufu Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ ikiwa ni siku chache tangu alipotekwa na baadaye kupatikana.
Mo (43), alitekwa alfajiri ya Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Osterbay jijini Dar es Salaam na kupatikana baada ya siku tisa katika maeneo ya Gymkhana alikotelekezwa na watekaji, huku pia wakitelekeza gari aina ya Toyota Surf walilolitumia likiwa na silaha kadhaa za moto.
Akizungumza na Mwananchi jana, kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema wamemwongezea ulinzi mfanyabiashara huyo katika kipindi hiki ambacho bado wanaendelea na uchunguzi.
“Ni kweli kwa kipindi hiki ambacho bado tunaendelea na uchunguzi, tumemwongezea ulinzi,” alisema Mambosasa.
Hali ofisini kwa Mo
Mwandishi wetu aliyefika katika ofisi za mfanyabiashara huyo katikati ya jiji aliambiwa na walinzi wa ofisi hizo kuwa bado hajaanza kazi.
Walinzi hao ambao hawakutaja majina yao, walisema tangu tukio hilo litokee ulinzi umeimarishwa nyumbani kwake na baba yake (Gullam Hussein Dewji) amepatiwa ulinzi binafsi na hata dereva anayewaendesha watoto kuwapeleka shule naye ana ulinzi maalumu tofauti na zamani.
“Baba yake (Mo) ndiye ambaye amekuwa akija ofisini, lakini naye maisha yamebadilika anakuwa na watu wasiopungua wawili kama wasaidizi,” alisema mmoja wa walinzi hao.
Alisema tofauti na zamani, Gullam alikuwa akizungumza na watu bila tahadhari yoyote, lakini sasa amekuwa akitembea na walinzi kila anakokwenda.
“Anapofika hapa hata jinsi ya kumsogelea na kuzungumza naye imekuwa ngumu kutokana na walinzi hao kutangulia kukudaka kabla ya kukutana naye.”
Hata hivyo alipotafutwa kufafanua jambo hilo, Gullam hakuwa tayari kuzungumzia, bali alijibu kuwa muda huo alikuwa na wageni.
Mbali na Mo na familia yake kuimarishiwa ulinzi, Mwananchi pia lilishuhudia uwekaji wa kamera za ulinzi (CCTV) katika Hoteli ya Colosseum ambako mfanyabiashara huyo alitekwa.
Siku lilipotokea tukio hilo, kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mambosasa alisema kamera za hotelini hapo zilishindwa kuonyesha picha za tukio hatua iliyoibua wasiwasi kwamba huenda zilikuwa zimechezewa.
Mwananchi liliwashuhudia mafundi jana saa nne asubuhi wakifunga kamera.
“Hizi kamera zimeanza kufungwa wiki iliyopita na leo ni kama siku ya tano, wameanza kuzifunga nyuma ya hoteli na kwenye maeneo ya nguzo,” kilieleza moja ya chanzo chetu.
“Tukio hili la kutekwa kwa Dewji limewachanganya akili sana menejimenti ya hapa hotelini, hata walinzi wameongeza ukaguzi, zamani walikuwa hawachukui details (taarifa) nyingi za gari ila sasa hivi naona kuna mabadiliko.”
Hata hivyo, uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Katika akaunti yake ya Twitter jana, Mo alitoa matumaini kwa klabu ya Simba aliyowekeza akiandika, “Tumefika hatua nzuri ya maendeleo ya uwanja wetu wa mazoezi wa #SIMBA. Nafurahi kuona maono yangu yanakamilika ili hata siku nisipokuwepo duniani uwanja uendelee kutumika kwa mazoezi Insha’Allah.”
Imeandikwa na Elias Msuya, Kelvin Matandiko na Khatim Naheka
Mwananchi

Comments