HRW: Saudia imruhusu mtoto wa Khashoggi kuondoka nchini humo.

HRW: Saudia imruhusu mtoto wa Khashoggi kuondoka nchini humoShirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, serikali ya Saudi Arabia inapaswa kumruhusu mwana wa kiume wa mwandishi na mkosoaji wa nchi hiyo aliyeuawa ndani ya ubalozi wa Saudia mjini Istanbul huko Uturuki, Jamal Khashoggi kuondoka nchini humo.

Mkurugenzi wa Human Righrs Watch kanda ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Michael Beach amesema kuwa ni kitendo kibaya na cha kutisha sana kwa serikali ya Saudia kumzuia Salah bin Jamal Khashoggi kuondoka nchini humo na kwenda nje ya nchi hiyo. 
Michael Beach ameongeza kuwa, kuna udharura wa kuishinikiza serikali ya Saudia ili imruhusu Salah bin Khashoggi kuondoka nchini humo kwa sababu pia ni raia wa Marekani. 
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pia wanapaza sauti zao wakiitaka Saudi Arabia iiruhusu familia ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi kuondoka Saudia. 
Mhariri wa gazeti la Washington Post, Karen Attieh ambaye alikuwa akifanya kazi pamoja na Jamal Khashoggi katika gazeti hilo amesema Jamal aliwahi kumwambia kwamba, jambo linalomhuzunisha sana ni kuona serikali ya Saudia ikiwazuia watoto wake kuondoka nchini humo na kujiunga naye nchini Marekani. 
Utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umechukua hatua ya kimaonyesho na kumpeleka mtoto wa Khashoggi, Salah katika kasri la Mfalme Salman bin Abdul Aziz kwa ajili ya eti kuwapa mkono wa pole kutokana na mauaji ya baba yake. 
Hata hivyo wadadisi wa mambo wanasema picha za mkutano huo zinaeleza kila kitu baada ya Salah bin Khashoggi kuonekana mwenye hasira na chuki wakati alipokutana na Mfalme Salman na mwanaye, Muhammad. 
Serikali ya Saudi Arabia imekiri kwamba, maafisa wa nchi hiyo wamehusika na mauaji ya Jamal Khashoggi katika ubalozi wa Saudia huko Istanbul.   
parstoday.

Comments