Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed
Shein, ametaka Watanzania kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote miongoni
mwao huku wakidumisha umoja na mshikamano miongoni mwao.
Pia
amewataka Watanzania wawapuuze watu wanaobeza Muungano kwa lengo la
kubaguana kwa kuwa wanaweza kusababisha mpasuko miongoni mwa Watanzania.
Dk.
Shein aliyasema hayo mjini Tanga jana wakati wa kilele cha sherehe za
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 zilizofanyika pamoja na maadhimisho ya
kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.
Alisema
Watanzania hawana budi kuzingatia sifa za msingi za kudumisha umoja na
mshikamano zitakazofanya jamii iendelee kumuenzi Baba wa Taifa kwa
vitendo.
“Hayati
Baba wa Taifa, katika falsafa zake alikuwa anasema watu ndiyo msingi wa
maendeleo badala ya kutegemea matumizi ya fedha kuwa msingi wa
maendeleo.
“Msingi
wa maendeleo ni watu wanaojituma kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu
katika kuleta maendeleo ya taifa lao na hayo ndiyo yalikuwa maono yake
Hayati Baba wa Taifa,”alisema Rais Dk. Shein.
Aliwataka
wananchi kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wahakikishe
wanajituma na kuwa wabunifu kuweza kuleta maendeleo ya haraka.
“Serikali
itahakikisha inasimamia rasilimali zake zote kwa karibu ziweze kutumika
kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania wote kwa ujumla na kwa kufanya
hivyo, tutakuwa tunamuenzi Baba wa Taifa.
“Kama
viongozi na wananchi wataweza kuzingaitia wosia wa Baba wa Taifa wa
kupinga rushwa kwa vitendo na kujiendeleza katika uchumi nchi hii
itaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Wakati wa uhuru, rais alipania kujenga nchi yenye amani ikiwamo kuheshimu misingi ya utu na kuhamasisha upendo miongoni mwetu.
“Kwa hiyo, kama tutaizingatia misingi hiyo, tutaweza kuleta mshikamano miongoni mwetu,” alisema.
Akizunguzia
elimu, Rais Dk. Shein alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo kwenye
sekta ya elimu kwa kuendelea kufanya maboresho mbalimbali kuleta
mabadiliko ya haraka.
“Tumejizatiti
kutoa elimu bora bila ubaguzi kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu
kwa sababu kwa kufanya hivyo kutasaidia vijana wetu kupata fursa ya
elimu na kuweza kujiajiri.
“Kupitia
elimu ndipo nchi itaweza kuzalisha wataalamu mahiri watakaoweza
kutafuta ufumbuzi wa majanga kama Ukimwi, rushwa na vitendo vyote
vibaya,” alisema.
Wakati
huo huo, aliwaasa vijana kupenda kufanya kazi na wasione aibu kwa
kuchagua kazi za maendeleo zinazojitokeza kwa sababu taifa linawategemea
wao kwa ajili ya kuiendesha nchi.
Kuhusu
mwenge wa uhuru, Rais Dk. Shein alisema mbio za mwenge huo zinaendelea
kuenziwa kila mwaka hata baada ya utawala wao kwisha.
Comments