RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa (UN)
katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kueleza kuwa kuanzishwa
kwa “Program ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP) itakuwa ni kichocheo cha mafanikio.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar
wakati alipokuwa na mazungumzo na Mratibu mpya wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa
eneo la Zanzibar Bi Dorothy Temu-Usiri.
Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na uzoefu mkubwa wa
utendaji kazi wa Mratibu huyo ana matumaini makubwa kuwa program hiyo sio tu
itasaidia kuimarisha maendeleo ya Zanzibar bali itasaidia sana katika kufikia
malengo ya maendeleo yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN) hapa nchini.
Rais Dk. Shein alisema kwamba, malengo ya Mashirika ya Umoja
wa Mataifa kwa Zanzibar yako wazi katika kila sekta na yanafahamika kwa
wananchi wote wa Zanzibar jinsi yalivyolenga katika kuimarisha sekta za
maendeleo.
Alisema kuwa (UN) imekuwa ikifanya kazi na kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali
ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, utawala bora,
uimarishaji wa haki za binaadamu, uwezeshaji, mapambano ya udhalilishaji wa
kijinsia pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Mashirika
ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa mashirikiano inayotoa katika kuimarisha miradi
mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar hasa katika masuala ya wanawake na
watoto.
“Programu ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP), inayohusisha
Mashirika tisa ya UN, aliizindua Rais Dk. Shein hivi karibuni hapa Zanzibar
ambapo katika uzinduzi huo alisisitiza haja kwa wafanyakazi kuleta mabadiliko
ya fikra na mawazo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuweza kuifanikisha
progamu hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alimuhakikishia Mratibu
huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na viongozi wake itaendelea
kutoa mashrikiano makubwa kwa Umoja huo pamoja na viongozi wake wote wakiwemo
wale wanaofanya kazi zao katika ofisi za Umoja huo hapa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa Programu ya pamoja ni mradi wa kipekee
unaolenga kuwawezesha watoto, vijana na wanawake hivyo ni matumaini yake
makubwa kuwa malengo yaliokusudiwa yatafikiwa kwa lengo la kutatua changamoto
zilizopo.
Comments