Baada ya Mbunge wa Jimbo
la Ukerewe mkoani Mwanza kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Joseph Michael Mkundi kutangaza kujiuzulu na kuomba kujiunga
na Chama cha Mapinduzi (CCM) usiku wa jana Oktoba 10, CHADEMA
wamekanusha tuhuma alizozitoa dhidi ya chama hicho.
Kupitia
barua aliyomwandikia Spika wa Bunge Job Ndugai, Mkundi amesema kuwa
amechukua uamuzi huo baadaya kutopatiwa ushirikiano na chama chake
katika maafa ya kuzama kwa kivuko cha Mv. Nyerere kilichopelekea vifo
vya watu zaidi ya 230.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo
ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amesema kuwa Mbunge huyo alipatiwa
ushirikiano ikiwemo wabunge kuchanga michango na kufika kisiwani Ukara.
"Wabunge walitoa rambirambi zao pamoja na kufika kwenye eneo la tukio pamoja na baadhi ya viongozi labda yeye aseme kama alitaka nani na nani wafike huenda kuna watu alitaka wafike na hawakufanya hivyo", amesema Mrema.
Mrema ameongeza kuwa chama kimeshangazwa na tuhuma hizo
na wamejaribu kumtafuta lakini hakupokea simu na baadae hakupatikana
tena, na kusema kuwa wanamtakia kila la heri katika maisha yake mapya
anayokwenda kuanza huko aendako.
Katika
barua yake kwa Spika wa bunge ya kujiuzulu uwanachama wa chama chake
cha zamani (CHADEMA) na kujiuzulu nafasi yake ya Udiwani na Ubunge,
amedai kuwa Chama chake cha zamani (CHADEMA) kimepoteza heshima na utu
baada ya kumtelekeza katika kipindi ambacho alihitaji msaada na
ushirikiano kutoka kwenye chama hicho na uongozi wake katika kipindi cha
msiba wa ajali ya Kivuko cha MV Nyerere, iliyotokea Septemba 20, 2018.
Mpekuzi.
Comments