Akizungumza kwa niaba ya waziri huyo, katika sherehe za miaka 20 za skuli ya Trifonia Academy, ziliyofanyika Fuoni, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, alisema serikali inathamini mchango unaotolewa na sekta binafsi katika uimarishaji wa elimu pamoja na kusaidia kuongeza wataalamu.
Hata hivyo, alisema ili malengo hayo yatimie, walimu hawana budi kujitolea katika kuwalea na kuwasomesha vizuri wanafunzi wao.
Aliwashauri walimu kuhakikisha wanajifunza mbinu mpya za ufundishaji ambazo zitamsaidia mwanafunzi hasa kwa masomo ya sayansi ambayo yanakimbiwa na wanafunzi wengi.
“Jitahidini kuzalisha vipaji vingi vyenye uwezo na utaalamu wa kuingia katika ushindani wa soko la ajira hasa kwa upande wa masomo ya sayansi,” alisema.
Alisema serikali inaendeleza juhudi za utatuzi wa changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa walimu wa sayansi pamoja na kuimarisha maslahi yao.
Aliwahimiza walimu kujenga utamaduni wa kubadilishana ujuzi pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano baina yao, wazazi na walezi.
Alitoa wito kwa skuli binafsi kufuata utaratibu wa usajili na ukataji leseni kwa wakati kwani wizara haitamvumilia mmiliki wa skuli ambayo haijasajiliwa.
Zanzibarleo.
Comments