Balozi Seif: Uzembe chanzo kikubwa cha ajali.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi, amesema uzoefu unaonesha ajali nyingi zinazotokea nchini chanzo chake ni uzembe na ukiukwaji wa makusudi wa sheria za usalama wa vyombo vya usafiri.

Alisema hayo wakati akiaghirisha mkutano wa 11 wa Baraza la tisa la wawakilishi, Chukwani Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Hivyo aliwataka wananchi wanaomiliki vyombo vya usafiri kufuata sheria za usalama wa abiria ili kunusuru maisha ya wananchi na mali zao.

Alisema serikali itaendelea kusimamia sheria za usalama wa vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu bila ya kumuonea muhali mtu yeyote.

Aidha kwa mara nyengine aliwaomba wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka katika maeneo hayo, ili kuondoa uwezekano wa kutokea maafa yanayoweza kutokea.

Kuhusu udhalilishaji, alisema jamii inayowadhalilisha wanawake na watoto, haiwezi kupata maendeleo ya haraka na hukosa thamani na heshima mbele ya macho ya jamii nyengine.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya akina baba wanaacha jukumu lao la malezi na badala yake kujiingiza katika kundi la wadhalilishaji wa watoto wa damu au wale wanaowalea.

Alisema vitendo hivyo ni vya kinyama na vya aibu kwa jamii yenye kufuata mila, desturi, silka na utamaduni.

Hivyo aliwaomba wazee wenye hulka kama hiyo wabadilike ili kuwapa faraja watoto wao wanaopaswa kupata furaha na amani katika maisha yao ya kila siku.

Alitanabahisha kwamba ulezi wa zamani wa kuwaacha watoto peke yao nyumbani umepitwa na wakati kwani unatoa fursa kwa wahalifu kuitumia nafasi kama hiyo kutekeleza vitendo vyao viovu.

Zanzibarleo.

Comments