Walisema Zanzibar ni kitovu cha utalii na inaingia wageni wengi hivyo ni vyema serikali kuwa makini na wageni hao.
Walitoa kauli hiyo ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati wakichangia ripoti ya utekelezaji wa ushauri wa kamati ya sheria, utawala bora na idara maalum za SMZ.
Ali Suleiman Ali Shihata (Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele) alisema, wakati umefika wa kuvitumia vitambulisho vya taifa na mzanzibari kuwabaini wageni wanaoingia nchini.
“Tuangalie vyema wageni wanaoingia kwenye shehia, yamejitokeza mambo mengi ya uhalifu hivyo tunapaswa kujiridhisha dhamira zao,” alisema.
Kuhusu usafi, alisema bado mazingira ya miji ya Zanzibar hairidhishi hasa ikizingatiwa kuwa ni kitovu cha utalii.
Mwakilishi wa jimbo la Tunguu, Simai Mohammed Saidi, alisema wageni wanaoingia wako chini ya dhamana ya serikali hivyo ni vyema kulinda usalama wao.
Akizungumzia wafanyakazi wa hotelini na nyumba za kulaza wageni, alisema ni vizuri kupatiwa vitambulisho ili kulinda usalama kwa wageni wanaowahudumia.
Aidha aliishauri serikali kuzifanyia matengenezo barabara za kijiji cha Nungwi kwani zinatumiwa na wageni na ni sehemu ya utalii.
Mapema akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa ushauri wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za SMZ, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri, alisema wapo wageni wanaoingia katika shehia bila kufuata utaratibu.
Zanzibarleo.
Comments