Kamati ya Bunge Yaitaka Serikali Kuzifanyia Marekebisho Sheria Ndogo Zinazokinzana na Katiba ya Nchi.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, inayoongozwa na mwanasheria mkongwe
na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, imeitaka Serikali
kubadilisha na kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria ndogo ili
ziendane na sheria mama za nchi kwani nyingi zinakinzana.
Chenge
akiwasilisha bungeni jana taarifa ya uchambuzi wa sheria ndogo
zilizowasilishwa kwenye mkutano wa 10 na 12 wa Bunge, alisema kamati
yake ilibaini baadhi ya kanuni zilizotungwa na wizara zinakwenda kinyume
na masharti yaliyowekwa na sheria mama au sheria nyingine za nchi.
Alitaja baadhi ya mapungufu ya kanuni hizo kuwa ni pamoja na kuweka mikokoteni.
Alisema
kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria kinasema sheria
ndogo yoyote inapaswa kutokiuka masharti ya Sheria ya Bunge inayotoa
mamlaka ya kutungwa kwake au sheria nyingine yoyote.
Sheria
alizosema zinakinzana na sheria mama ni Sheria ya Mafuta na Gesi,
Sheria ya Madini, Kanuni ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Sheria
ya Mipango Miji.
Akizungumzia
sheria hiyo, Chenge alisema ina masharti yanayokinzana na sheria mama
ambapo katika kanuni ya 3 inayotoa tafsiri ya neno ‘vehicle’ ikihusisha
vitu kama mkokoteni wa kuvutwa na ng’ombe, baiskeli ya matairi mawili na
baiskeli ya matairi matatu (guta) ambapo tafsiri hiyo ni kinyume na ile
inayotolewa na Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168.
Alisema
sheria hiyo haijabainisha vifaa hivyo kuwa ni sehemu ya vyombo vya moto
ambapo masuala hayo kwa namna yoyote ile hayahusiani na maudhui ya
kanuni hiyo inayohusu masuala ya mipango miji.
“Kamati
ilifanya uchambuzi na kubaini kanuni ya 3 inatoa tafsiri ya neno jengo
kuwa inahusisha pia mabango ya matangazo na minara ya simu kinyume na
tafsiri inayotolewa na sheria mama chini ya kifungu cha 2 ambayo pamoja
na masuala mengine haijafafanua masuala ya mabango ya matangazo na
minara ya simu,” alisema.
Akizungumzia
sheria hiyo, Chenge alisema uchambuzi ulibaini Kanuni ya 4 (2) (b) ya
kanuni hizi inampa Waziri wa Fedha jukumu la kushiriki katika
majadiliano ya mikataba ya kugawana mapato katika sekta ndogo ya mafuta
na gesi asilia nchini.
“Kamati
inaona kanuni hii imemuongezea Waziri wa Fedha majukumu mapya ambayo
hayatajwi katika kifungu cha 4 cha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya
Mafuta na Gesi, sura ya 328.
“
Kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 47 vya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015,
majukumu ya yanayoainishwa na kanuni husika yanapaswa kutekelezwa na
Waziri wa Nishati, TPDC na PURA kwa niaba ya Serikali ambapo majukumu
haya hayaingiliani na yale ya Waziri wa Fedha chini ya Sheria ya
Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi,” alisema.
Kuhusu
Sheria ya Madini, Chenge alisema kamati imebaini dosari katika kanuni
ya 3 inayotoa tafsiri ya neno Kampuni ya Mzawa/Wazawa kuwa ni ile
inayomilikiwa kwa asilimia 51 na Mtanzania/Watanzania na ina asilimia 80
ya Watanzania katika nafasi za watendaji wa juu.
“Tafsiri
inayotolewa katika kanuni hii haipo katika Sheria ya Makampuni Sura ya
212 ambayo ndiyo sheria mama inayosimamia masuala yote ya kampuni
nchini.
“Utaratibu
wa kuanzisha tafsiri mpya ya maneno ni vema ukaanzia katika Sheria Mama
au Sheria nyingine ya nchi ambayo ni mahsusi kwa jambo fulani, hii
itasaidia kuondoa uwezekano wa kuwa na mkanganyiko wa tafsiri za maneno
mbalimbali,” alisema Chenge.
Alisema
katika kanuni ya sheria hiyo pia tafsiri ya neno Kampuni ya
mzawa/wazawa na Benki ya Watanzania wazawa iliyotumika katika kanuni
hiyo ina ukakasi.
“Pamoja
na nia njema ya wizara ya Madini ya kuweka tafsiri hizo, utekelezaji
wake una changamoto na unaweza ukawa na matokeo hasi kwa kampuni kama
Puma Energy ambapo Serikali inamiliki asilimia 50 ya hisa zote na kwa
Benki ya NBC Ltd, ambapo Serikali inamiliki asilimia 15 ya hisa zote.
“Sheria
ndogo hiyo haitambui umiliki wa Serikali wa hisa katika benki ya NBC na
katika Kampuni ya Puma kuwa ni umiliki wa Watanzania na hivyo
kuzikosesha kampuni hizo fursa ya kushiriki kiuchumi katika sekta ya
madini.
“Halikadhalika
benki na taasisi za fedha nyingi zilizosajiliwa hapa nchini ambazo
hazimilikiiwi na Watanzania kwa asilimia 100 au kwa hisa nyingi zitakosa
fursa ya kushiriki kwenye sekta ya madini, kamati haiamini kwamba haya
ndiyo yalikuwa madhumuni ya kutungwa kwa sheria hiyo,” alisema Chenge.
Mpekuzi.
Comments